Sakata la Tumbili 61 Waliokamatwa Uwanja wa Ndege Lachukua sura Mpya - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Saturday, 26 March 2016

Sakata la Tumbili 61 Waliokamatwa Uwanja wa Ndege Lachukua sura Mpya


Serikali imeunda kikosi kazi kinachohusisha taasisi nyeti nchini kuchunguza sakata la kukamatwa kwa raia wawili wa Uholanzi wakiwa katika harakati za kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Albania.

Kikosi hicho kinaundwa na maofisa kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Kikosi cha Kupambana na Ujangili.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa aliwathibitishia wanahabari jana kuundwa kwa kikosi kazi hicho na kwamba, upelelezi wa sakata hilo umepamba moto.

“Upelelezi ndiyo kwanza bado mbichi, kwa hiyo siwezi kusema lolote kama lini watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa sababu upelelezi uko chini ya kikosi kazi hicho,” alisema Mutafungwa.

Juzi saa tano asubuhi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alitembelea Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kushuhudia wanyama hao.

Profesa Maghembe alisema kama kila kitu kitakwenda vizuri katika upelelezi, watuhumiwa wa kosa hilo watafikishwa mahakamani siku ya Jumanne.

Wanyama hao walikamatwa usiku wa kuamkia juzi katika uwanja huo wakati raia hao, Artem Alik Vardanyian (52) na Eduard Alik Vardanyian (44) wakiwa katika harakati za kuwasafirisha kwa kutumia ndege kubwa ya mizigo.


Hata hivyo, raia hao wa Uholanzi walikuwa na vibali vilivyotolewa na Mkurugenzi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Charles Mulokozi ambaye tayari amesimamishwa kazi kwa kashfa hiyo. 
Post a Comment