Polisi Wafanya Upekuzi Nyumbani Kwa Halima Mdee - LEKULE

Breaking

2 Mar 2016

Polisi Wafanya Upekuzi Nyumbani Kwa Halima Mdee


Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam jana lilifanya upekuzi mkubwa katika nyumba ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) baada ya kumtilia shaka kuwa na nyaraka muhimu za vikao vya uchaguzi wa Meya wa Jiji hilo.

Kikosi cha jeshi hilo kilifika katika nyumba ya mbunge huyo majira ya saa tisa alasiri na kufanya mazungumzo na Mwanasheria wake, John Mallya ambapo baada ya kukamilisha taratibu za kisheria walianza zoezi la upekuzi uliochukua zaidi ya saa moja.

Kiongozi wa kikosi hicho cha Polisi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa walilazimika kufanya upekuzi katika nyumba hiyo baada ya kusadikika kuwa wakati wa vurugu zilizotokea katika ukumbi wa Karimjee jijini humo wikendi iliyopita kufuatia kuahirishwa kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji, Mdee aliondoka na faili muhimu lenye madokezo yanayohusu uchaguzi huo.

Hata hivyo, baada ya kukamilisha upekuzi huo, Polisi walijiridhisha kuwa hakukuwa na nyaraka hizo ndani ya nyumba hiyo wala kitu chochote ambacho wangekitilia shaka licha ya kukuta nyaraka nyingi za mbunge huyo. Hivyo, walitoa cheti maalum cha kuthibitisha kuwa hakuwa na nyaraka zozote kinyume cha sheria.

“Wamekagua nyaraka zote. Madai yao ni kuwa Halima alimpora au alichukua nyaraka za kiongozi wa Jiji, lakini wamekuta hakuna jambo lolote ambalo linatiliwa shaka. Na wametoa Certificate inayoonesha kwamba hakuna chochote ambacho kimechukuliwa,” alisema Mwanasheria wa Mbunge huyo, John Mallya.

Mdee alishikiliwa na Polisi na kulala rumande juzi kutokana na tuhuma za kushiriki katika vurugu zilizotokea katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Jumamosi, Februari 27.


Wengine wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi ni Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.

No comments: