Paul Makonda Amkataa Hakimu Anayesikiliza Kesi ya Kuwakashfu Makada Wenzake wa CCM.....Kubenea Naye Akutwa na Kesi Ya Kujibu Sakala la Kumtusi Makonda - LEKULE

Breaking

4 Mar 2016

Paul Makonda Amkataa Hakimu Anayesikiliza Kesi ya Kuwakashfu Makada Wenzake wa CCM.....Kubenea Naye Akutwa na Kesi Ya Kujibu Sakala la Kumtusi Makonda



Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda jana alitinga mahakamani na kumkataa hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi iliyofunguliwa dhidi yake na makada wawili wa zamani wa CCM wanaodai aliwakashifu.

Kesi dhidi ya Makonda, ambayo awali ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Hellen Liwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilishafikia hatua ya utetezi na Makonda alitakiwa kuanza kujitetea jana, baada ya mahakama hiyo kumuona kuwa ana kesi ya kujibu.

Hata hivyo, jana Makonda ambaye alifika mahakamani kwa mara ya kwanza tangu kesi hiyo ilipofunguliwa, alishikilia msimamo wa kutokuwa na imani na hakimu huyo na hivyo kuomba apangiwe hakimu mwingine.

Makonda alifikia msimamo huo kutokana na maneno aliyoelezwa na wakili wake, ambayo kwa mtazamo yalionyesha kuwa hakimu atakuwa anawapendelea wadai na hivyo asingemtendea haki.

Kutokana na madai ya Makonda, Hakimu Liwa amejitoa kwenye kesi hiyo na amepanga ianze kusikiliza upande wa mashtaka Machi 23.

Kesi dhidi ya Kubenea 
Wakati Makonda akimkataa hakimu, mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea ameonekana ana kesi ya kujibu katika kesi inayomkabili ya tuhuma za kumtukana mkuu huyo wa wilaya. 

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu anayesikiliza kesi hiyo, ikiwa ni siku chache baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake.

Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Simba alisema kuwa baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka uliotolewa na mashahidi watatu, aliridhika kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu.

Baada ya uamuzi huo wakili wa Kubenea, Peter Kibatala aliieleza mahakama kuwa mteja wake atajitetea kwa kiapo na kwamba watakuwa na mashahidi wanne na wanakusudia kuwaita wote mahakamani siku ya kujitetea.

Hakimu Simba alipanga mshtakiwa huyo aanze kujitetea Machi 7, mwaka huu.

Kubenea, ambaye alipandishwa kizimbani, mahakamani hapo Desemba 15, mwaka jana, anadaiwa kumtolea DC huyo lugha ya matusi Desemba 14 mwaka jana wakati wakiwa kiwanda cha Tooku Garments kilichoko Mabibo External, Kinondoni, jambo ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Anadaiwa kuwa siku hiyo alimuita Makonda kuwa ni “kibaka, mpumbavu na mjinga” na kwamba cheo chenyewe cha ukuu wa wilaya ni cha kupewa.

Wakati wa ushahidi wake, Makonda aliieleza mahakama kuwa alitumia nafasi yake ya ukuu wa wilaya kwenda kiwandani kwa lengo la kuzungumza na wafanyakazi waliokuwa wamegoma.

Mashahidi wengine wa upande wa mashtaka walikuwa ni maofisa wa polisi waliokuwapo eneo la tukio siku hiyo.

Alisema alipomaliza kuzungumza na wafanyakazi hao na kufunga kikao hicho, wakati anageuka alishangaa kumsikia mshtakiwa akimtukana.

No comments: