Kilichotokea CRDB Mbagala Jijini Dar leo karibu na benki iliyovamiwa na Majambazi mwezi uliopita - LEKULE

Breaking

11 Mar 2016

Kilichotokea CRDB Mbagala Jijini Dar leo karibu na benki iliyovamiwa na Majambazi mwezi uliopita

 NA K-VIS MEDIA/Khalfan Said
POLISI wamelazimika kufyatua mabomu ya machozi ili kuwatawanya watu waliojikusanya mbele ya Benki ya CRDB tawi la Mbagala - Rangi Tatu, baada ya mtu mmoja aliyekuwa akiongea na simu ndani ya benki hiyo kukaidi maagizo ya polisi ya kuacha kufanya hivyo mapema leo mchana wa Machi 11, 2016.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, watu watatu mmoja akiongea na simu na wengine wawili waki-chat ndani ya benki hiyo, waliagizwa na mlinzi wa benki kuacha kufanya hivyo lakini wakakaidi.

Baada ya mlinzi kuona hivyo alitoa taarifa kituo cha polisi Mbagala - Maturubai, na hapo polisi wakiwa ndani ya gari lao maarufu kama defender, waliwasili kwenye eneo hilo na kuamuru watu hao ambao wanaelezwa kuwa wateja, kutoka ndani ya benki hiyo.

Hata hivyo palitokea mabishano baada ya mmoja wao kukaidi amri ya polisi na kuanza kupigana nao.
 
Kuona hivyo watu walianza kujaa na polisi bila kufanya ajizi wakafyatua mabomu ya machozi kutawanya watu na kuwadhibiti 'wateja' hao wabishi na hatimaye kufanikiwa kuondoka nao.


Hali hiyo ilizua tafrani huku watu wakidhani kuwa palikuwepo na tukio la ujambazi, kwani ni mwezi uliopita umbali wa mita chache kutoka kwenye benki hiyo, palitokea tukio baya ya uvamizi wa benki ya Access ambapo watu saba waliauawa, wakiwemo polisi.

No comments: