Kamati ya Bunge Yaipa Siku 7 Wizara ya Afya Ieleze Kwa nini Watumishi wa Hospitali ya Butimba Walisimamishwa Bila Kufuata Utaratibu - LEKULE

Breaking

18 Mar 2016

Kamati ya Bunge Yaipa Siku 7 Wizara ya Afya Ieleze Kwa nini Watumishi wa Hospitali ya Butimba Walisimamishwa Bila Kufuata Utaratibu

Kamati ya bunge ya huduma za jamii imeitaka Wizara ya Afya ijieleze ndani ya siku saba kwanini aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, aliwasimamisha watumishi wa Afya wa hospitali ya Butimba bila kufuata hatua stahili.

Mapema mwezi huu, Magesa Mulongo aliwasimamisha kazi madaktari 3, manesi 6, na wafanyakazi wengine 2 wa hospitali ya Butimba kwa madai mbalimbali, yakihusisha kifo cha watoto mapacha. Lakini Mulongo alijitetea maamuzi yake kuwasimamisha, akisema ilitokana na tendo walilofanya kutoendana na sheria za kazi.

Mwenyekiti wa kamati Raphael Chegeni, alisema kamati iligundua kwamba kulikuwa na matumizi mabaya ya madaraka katika maamuzi ya mkuu wa mkoa. Na kwamba mkuu wa mkoa hakuomba taarifa ya utenda kazi ili kutambua matatizo ya hospitali.

Mmoja wa wanakamati Mhe. Zitto Kabwe ndiye aliuliza ni kitu gani hasa kilichosababisha mkuu wa mkoa kusimamisha watumishi hao, kwani kuna wagonjwa wengi wanaofariki katika hospitali husika kwa kukosa tiba na wengine wakiwa na shida mbalimbali.

Raphael Chegeni alisema mkuu wa mkoa hakufuata kanuni, zinazohitaji watumishi wa afya kusimamishwa na mabaraza yao.

"Kamati imejiridhisha kwamba mkuu wa mkoa aliwasimamisha wafanyakazi hawa wa afya kwa kutumia nguvu ya kisiasa" alisema Raphael Chegeni. Pia alionya wanasiasa, kuchanganya siasa na utoaji wa huduma za afya, hususani maeneo ya vijijini, kwani mwisho wa siku itawaamiza wakaazi wa vijijini.

Akichangia, mbunge wa viti maalumu, Mhe. Suzan Lyimo alisema viongozi wa serikali wanapaswa kutambua mchango wa watumishi wa afya wanaofanya kazi kubwa kuokoa maisha.


Kamati pia ilishauri wizara kuboresha mazingira ya kazi ya wafanyakazi wa afya, ikiwa ni pamoja na kuboresha mishahara na marupurupu.

No comments: