Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Lampongeza Rais Magufuli Kwa Kutumia Lugha Ya Kiswahili Kwenye Mikutano ya Kitaifa na Kimataifa - LEKULE

Breaking

14 Mar 2016

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Lampongeza Rais Magufuli Kwa Kutumia Lugha Ya Kiswahili Kwenye Mikutano ya Kitaifa na Kimataifa

Na Lorietha Laurence- MAELEZO

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa uzalendo wake wa kuitumia lugha ya Kiswahili katika mikutano mikubwa na hafla mbalimbali za kitaifa na kimataifa.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi BAKITA, Prof. Martha Qorro ameeleza msimamo huo wa Rais Dkt.Magufuli  umewasidia Watanzania kupata taarifa moja kwa moja kutoka tukio husika.

“Uamuzi na msimamo wa Rais Magufuli wa kutumia lugha ya Kiswahili katika mikutano mikubwa ikiwemo  mkutano mkuu wa 17 wa viongozi wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepokelewa kwa furaha kubwa na wananchi na wadau wengi wa Kiswahili ndani na nje ya Tanzania” alisema Prof.Martha.

Aliongeza kuwa kupitia msimamo huo wa Mhe. Rais Magufuli,   Baraza linaamini kwamba hatua hiyo itasaidia kukuza lugha ya Kiswahili na kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania kupitia tafsiri na ukalimani na hivyo kuwapelekea maendeleo wananchi wote wa Afrika Mashariki.

Naye Katibu Mtendaji wa BAKITA Dkt. Seleman Sewangi ametoa wito kwa viongozi wengine wa ngazi mbalimbali za Kitaifa kufuata nyao za Mhe.Rais Magufuli kwa kuipa kipaumbele lugha ya Kiswahili ili kufikisha ujumbe kwa Watanzania walio wengi.

“Natoa wito kwa viongozi wetu wa ngazi mbalimbali za kitaifa kuitumia lugha ya Kiswahili katika mikutano mikubwa na hafla mbalimbali za kitaifa na kuachana na dhana ya kutumia lugha ya kigeni yenye lengo la kuwafurahisha wageni wachache” alisema Dkt. Sewangi.

Aidha, aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa lugha ya kiswahili inatumiwa vizuri, Baraza hilo linaendelea kutekeleza mkakati wa kukamilisha kanuni zitakazopelekwa bungeni ili kumuwezesha Waziri mwenye dhamana kuwa na mamlaka ya kusimamia sheria ya lugha ya Kiswahili ya mwaka 1961 iliyorekebishwa mwaka 1985 ili kuipa nguvu ya kumshitaki mtu yeyote kwa matumizi mabaya ya lugha hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi,Taasisi ya Taaluma za Kiswahili chuo kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Ernesta Mosha ameziomba ofisi za Serikali hususani mahakama kutumia lugha ya Kiswahili kwa kuwa ni lugha inayoeleweka na Watanzania wengi ikizingatiwa kuwa sio wote wanajua kutumia lugha ya kiingereza.

No comments: