ZEC Yagoma Kuondoa Picha ya Maalim Seif Kwenye Karatasi za Kura........CUF Yasema Ipo Tayari Kwa Mazungumzo ila Sio Kurudia Uchaguzi - LEKULE

Breaking

13 Feb 2016

ZEC Yagoma Kuondoa Picha ya Maalim Seif Kwenye Karatasi za Kura........CUF Yasema Ipo Tayari Kwa Mazungumzo ila Sio Kurudia Uchaguzi

Zikiwa  zimebaki siku chache kabla ya kurudiwa kwa uchaguzi Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharrif Hamad amehoji sababu za chama tawala, CCM kuhofia CUF kuongoza visiwa hivyo.

Maalim Seif, ambaye aligombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25 ambao matokeo yake yalifutwa, pia amesema endapo CCM itasitisha uchaguzi huo uliopangwa kufanyika siku 36 zijazo, CUF watakuwa tayari kufanya mazungumzo lakini si kwa wakati huu ambao maandalizi ya kupiga kura yanaendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, katibu huyo mkuu wa CUF aliitoa hofu CCM kuwa chama chake hakina ajenda ya kulipiza kisasi.

Matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani yalifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha siku ambayo chombo hicho kilitakiwa kumtangaza mshindi, na mwezi uliopita alitangaza Machi 20 kuwa siku ya uchaguzi wa marudio visiwani humo.

Wakati CUF ikipinga vikali kufutwa matokeo na kutangaza tarehe mpya, Serikali imesema kuna nafasi ya kufanya mazungumzo kabla ya uchaguzi wa marudio kwa kuwa kuna muda  mrefu wa kufanya hivyo.

Jecha alitangaza uamuzi huo wakati tayari matokeo ya urais ya majimbo 31 yalishatangazwa, na ya majimbo tisa yaliyosalia yalishahakikiwa, huku washindi wa viti vya uwakilishi na udiwani wakiwa wametangazwa na kupewa vyeti vya ushindi. 
“Sijui kwa nini CCM wanaogopa sisi tukiongoza?” alihoji Maalim Seif kwenye mkutano huo na waandishi akiwa pamoja na aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.

“Wana wasiwasi gani, kwamba CUF ikiongoza kutatokea nini? Sisi hatuna ajenda ya kulipiza kisasi,” alisema.

Katika mkutano huo, Maalim Seif mbaye pia ni katibu mkuu wa chama hicho alisema kama CCM ina wasiwasi na idadi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), haina budi kuondoa shaka kwa kuwa idadi kwa pande zote inakaribiana.

“Hawa wanahisi hawatapata uwakilishi mkubwa, lakini mbona miaka yote tunakuwa na idadi isiyopishana ya wawakilishi?” alihoji.

Kuna Vitisho  Zanzibar 
Katika mkutano huo, Maalim Seif alisema kumekuwapo vitendo vya wananchi kupigwa na vikundi vya watu wasiojulikana. 
Alidai wafanyakazi wa Serikali na taasisi zake wameamrishwa kupeleka vitambulisho vyao vya kazi na vya kura serikalini ili vikahakikiwe.

“Hii si mara ya kwanza wafanyakazi wa Serikali kutakiwa kupeleka vitambulisho, sisi tunajua kuwa wanataka wawatishe kuwa watajua nani kapiga kura na nani hajapiga,” alisema na kusisitiza:
“Hii ni kama kitisho cha kuwalazimisha wakapige kura, zaidi hasa hizo ni dhuluma ambazo wananchi wanafanyiwa.”

Kadhalika Maalim Seif alizungumzia uwapo wa watu wanaovaa soksi usoni na kuwashambulia raia, akisema Serikali haijachukua hatua stahiki kudhibiti hali hiyo.

Alisema watu hao ambao wamepachikwa jina la mazombi, wamevamia maeneo kadhaa kama Baraza la CUF, Jang’ombe na yaleambayo yana wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani humo.

“Wanawapiga watu, wanawajeruhi na wanaiba mali, lakini inashangaza sana mambo haya na si Serikali wala polisi iliyochukua hatua,” alisema.

Maalim Seif alisema amezungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuhusu matukio hayo ya uharamia wanaofanyiwa wananchi, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

Alisema CCM wanatafuta sababu ili machafuko zaidi yatokee visiwani humo wapate kisingizio.

Aliwataka wafuasi wa CUF kuvumilia hali hiyo ili nchi isiingie kwenye machafuko kama yaliyotokea mwaka 2000, wakati watu zaidi ya 20 waliuawa na wengine kukimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya ambako waliishi kama wakimbizi.

 Lowassa Azungumza
Kwa upande wake, Lowassa aliwataka viongozi wa ngazi za juu wachukue   hatua kumaliza mgogoro wa Zanzibar.

“Hili tulichukulie kwa umakini sana. Viongozi wafanye vikao vya maridhiano, tunaipenda sana amani tuliyonayo,” alisema.

Lowassa alisema anashangazwa na jinsi CCM wanavyoshindwa kuheshimu makubaliano ya SUK na kukataa kukubali matokeo. 
ZEC  yagoma  kuondoa  picha  ya  Maalim 
Wakati huohuo, habari zinaarifu kuwa Tume  ya  Uchaguzi  Zanzibar( ZEC)  imegoma  kuondoa  picha  za  wagombea  Urais,Udiwani  na Uwakilishi  kutoka  vyama  vilivyotangaza  kutoshiriki  uchaguzi  wa  marudio,ikiwemo  jina  na  picha  Maalim Seif Sharif Hamad.
Hilo  lilifahamika  jana mjini Unguja  baada  ya  kigogo  mmoja  wa  ZEC ambaye  hakuwa  tayari  kutaja  jina  kusema  kuwa  sheria  hazimruhusu  mgombea  yeyote  kujitoa  mwenyewe  kwa  utashi  wake  binafsi.
Kiongozi  huyo  alisema  kwa  mujibu  wa  kifungu  cha  36  cha  sheria  ya  uchaguzi  namba  11  ya  mwaka  1984,mgombea  hawezi  kujiondoa  kwa  utashi  wake  baada  ya  Tume  kukamilisha  kazi    ya  uteuzi  ambayo  ilifanyika  kabla  ya  Oktoba  25  mwaka  jana.

"Ieleweke  kwamba mgombea  urais  anaweza  kujiondoa  katika  kinyang'anyiro  kwa  kuwasilisha  taarifa  za  maandishi  yeye  mwenyewe  ofisi  za  ZEC  kabla  ya  saa 10  jioni  ya  siku  ya  uteuzi." Alisema  ofisa  huyo  akinukuu  kifungu  cha  katiba.

Alisema  uteuzi  wa  mgombea  mwingine  unaweza  kufanyika  ndani  ya  siku 21  kama  mgombea  hatafariki dunia,lakini  hakuna  ruhusa  ya  kujitoa  kabla  ya  kukamilika  kwa  uchaguzi.

Alisema  ZEC  tayari  imeviandikia  vyama  kuvitaka  vithibitishe  iwapo  wagombea  wao  wangali  hai  au  kuna  waliofariki dunia, na si kutaka  kufahamu  kama  watashiriki  uchaguzi  wa  marudio  au  la.
Mkurugenzi  wa  Mipango  na  Uchaguzi CUF  anena
Mkurugenzi  wa  Mipango  na  Uchaguzi  wa  CUF, Omar Ali Shehe  amesema  ZEC  inasuka  mkakati  wa  siri  wa  kutaka  kuzitumia  picha  na  taarifa  za  wagombea wao  kwa  lengo  la  kuidanganya  dunia  na  jumuiya  za  kimataifa  kwamba  CUF  walishiriki  uchaguzi  huo.


Shehe  amesema  CUF  kilitangaza  mapema  kabisa  kutoshiriki  uchaguzi  wa  marudio,hivyo  dunia  nzima  inaelewa  kabisa  kwamba  CUF  haishiriki  uchaguzi  huo  na  kitendo  cha  kuendelea  kuchapisha  picha  na  taarifa  za  wagombea  wao  katika  karatasi  za  wapiga  kura  si  sahihi.

No comments: