Waziri Mkuu Asubiriwa Kwa Mabango Kiteto - LEKULE

Breaking

25 Feb 2016

Waziri Mkuu Asubiriwa Kwa Mabango Kiteto



Wananchi  wilayani Kiteto  mkoani  Manyara  wamejiandaa  kumpokea  kwa  mabango  Waziri  Mkuu  Kassim  Majaliwa  ili  kutoa  ujumbe  wa  kuwakataa  baadhi  ya  viongozi  wa wilaya  kutokana  na   kukithiri  kwa  migogoro  ya  ardhi.

Miongoni  mwa  viongozi  wanaotajwa kuwamo  katika  ujumbe  huo  ni  Mkuu  wa  Wilaya Kanali Samweli Nzoka, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Bosco Ndunguru,Katibu Tawala (DAS) Nicodemus John pamoja  na  kamanda  wa  Polisi  wa  Wilaya (OCD) George Katabazi.

Hata  hivyo DC Nzoka  amepiga  marufuku  mwananchi  yeyote  kuandaa  bango  lolote  katika  ziara  hiyo  ya  Waziri  Mkuu  inayotarajiwa  kufanyika  Februari  29  mwaka  huu.

Akizungumza katika kikao  cha  baraza la  Madiwani  jana,Nzoka  alisema  hataruhusu  kuandaliwa  wala kuonyeshwa  mabango  hayo  kwani  ni  ishara  ya  vurugu  na  uvunjifu  wa  amani.

Mkuu  huyo  wa  Wilaya  alisema  anazo  taarifa  za kuwapo  watu  walioandaliwa  kutoka  wilaya  na  mikoa  ya  jirani  kwenda  Kiteto  kuzomea baadhi  ya  viongozi  wa  Wilaya katika  ziara  hiyo.

Katika  ziara  hiyo, Majaliwa  atakutana  na  kuzungumza  na  viongozi  mbalimbali  wakiwemo  madiwani, wakuu  wa  idara  na  viongozi  wa  mila  wa  jamii  ya  wafugaji

Waziri  mkuu  anategemewa  kutoa suluhisho  la mgogoro  wa  ardhi  kati  ya  wakulima  na  wafugaji  uliodumu  kwa  muda mrefu  na kusababisha  mauaji.

No comments: