Waziri Kairuki Asema TAKUKURU Kuna Majipu Yanayohitaji Kutumbuliwa - LEKULE

Breaking

16 Feb 2016

Waziri Kairuki Asema TAKUKURU Kuna Majipu Yanayohitaji Kutumbuliwa



WAFANYAKAZI wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), wametakiwa kuanza kujisafisha huku wakiambiwa kwamba taasisi hiyo haitaepuka kutumbuliwa majipu.

Aidha, wameagizwa kuwasilisha upya taarifa za mali zao kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, zifanyiwe uhakiki wa mali; moja baada ya nyingine kubaini waliofanya udanganyifu wa umiliki wa mali zao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alisema hayo jana Dar es Salaam kwenye ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa viongozi wa taasisi hiyo.

Alisisitiza kuwa tayari anazo taarifa zinazohitaji baadhi ya viongozi wa taasisi hiyo kutumbuliwa majipu muda muafaka utakapowadia. 

Kairuki aliagiza taasisi hiyo kufanyia tathmini kesi zake zote, ilizowahi kushindwa na kuja na majibu ya sababu za kushindwa na endapo itabainika hazikushinda kutokana na mchezo mchafu wa wachunguzi, wahusika wachukuliwe hatua haraka iwezekanavyo.

“Niliposikia mnataja majina yenu wakati wa kujitambulisha, nilikuwa nafurahi sana kwani wengi wenu nawajua na nina taarifa zenu. Haiwezekani wewe mtu mmoja watu wengi wawe wanakuongelea vibaya. Msifikiri majipu humu (Takukuru) hakuna, yapo na nawahakikishia tutayatumbua tu,” alisisitiza Waziri huyo.

Alisema iwapo yupo mtumishi hasa viongozi wa taasisi hiyo, anayejitambua kuwa ni ‘jipu’, ajisalimishe kwani akiendelea kusubiri na kutumbuliwa, mwisho wake utakuwa mbaya. 

“Tukiwatumbua hali itakuwa mbaya kwani nyie mko chini ya Ofisi ya Rais, hata Rais (Dk John Magufuli) hatasita kuwachukulia hatua si tu za kinidhamu bali hata za kisheria,” alibainisha.

Alisema katika taasisi hiyo, yapo maeneo mengi yanayohitaji kutumbuliwa majipu kuanzia Uhasibu, Ukaguzi na Manunuzi zikiwemo ofisi za mikoani akitolea mfano Mkoa wa Kilimanjaro na makao makuu, Upanga, Dar es Salaam.

“Tutasafisha nawahakikishia hata ikibidi kuanza upya, ikitulazimu pia kufukuza wote ikithibitika mnakwenda kinyume na maadili yenu tutawafukuza ila hatutamwonea mtu, kwani wako watu wengi wenye sifa wanaotaka kufanya kazi,” alisisitiza Kairuki.

Alisema kuanzia sasa, ofisi hiyo itawekewa malengo ya utendaji wake na kufanyiwa tathmini hasa kwa kesi zilizoshindwa ifahamike aliyezifanya, sababu za kushindwa, iwapo imetokana na uzembe au kama upo mkono wa mtu. 

Alisema imefikia wakati sasa watumishi wa taasisi hiyo wanapaswa sasa wale kiapo cha ahadi ya uadilifu na kukisaini ili watakaoshindwa wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Taarifa za mali
Aliwataka watumishi wote wa taasisi hiyo, kurejea upya kuwasilisha taarifa za mali zao kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

 Alisema taarifa hizo zitapewa kipaumbele cha kuhakikiwa mali moja baada ya nyingine na endapo mtumishi atabainika kufanya udanganyifu wa mali anazomiliki, atachukuliwa hatua.

Alihadharisha kuwa chombo hicho cha kupambana na rushwa hakipaswi kutuhumiwa kwa rushwa. Alisema kikituhumiwa kwa sifa hiyo, ni sawa na kuigeuza Takukuru kuwa jipu badala ya vidole vya kutumbulia majipu.

Takukuru mpya
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano, imejipanga kuhakikisha inazalisha chombo kipya cha kuzuia na kupambana na rushwa chenye maadili. 

Aliwataka wanaoona hawawezi kwenda na kasi hiyo, wawasilisha barua zao za kujiuzulu kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Kamishna wa Polisi Valentino Mlowola.

Hata hivyo, alisema Serikali inatambua kuwa kazi ya upelelezi na uchunguzi ni ngumu kutokana na kukabiliwa na vishawishi vingi, jambo ambalo wanahitaji ujasiri. Alisisitiza watumishi hao kutunza heshima yao na chombo hicho.

“Faraja ya uchunguzi ni kufanikisha majalada kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na baadaye watuhumiwa kufikishwa mahakamani. Sasa ili kufanikisha faraja hii ni vyema kufanya kazi kwa weledi na tusiwe na pupa ili mradi tupeleke kesi nyingi kwa DPP na kuziwasilisha mahakamani,” alisema Kairuki.

Aliendelea, “Nasema haya kwa sababu nafahamu bado kwenye uchunguzi hapa Takukuru kuna upungufu. Nafikiri mmemuona Mheshimiwa Rais anavyoshughulikia suala la rushwa na ufisadi, ni wajibu wenu Takukuru kufanikisha azma hii kwa kuja na matokeo ya utendaji chanya.”

Aidha, waziri huyo aliitaka taasisi hiyo kutumia weledi, sifa yaa ukachero wa kiupelelezi na kiuchunguzi kufuatilia matukio yenye shaka yanayoendelea mitaani na si kusubiri taasisi kubwa kuyavumbua.

“Nyie ndio makachero tumieni ukachero wenu kuibua ufisadi, kuna mtu mmoja amebainishwa na Rais lakini jina lake kwa umaarufu na utajiri wake linatumika kama kituo, alishajiuliza sababu na kuchunguza?”alihoji.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mlowola aliwataka wafanyakazi wa taasisi hiyo kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea. 

Kasi ya Magufuli 
Aliwataka wahakikishe wanaendana na kasi ya Dk Magufuli na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya utendaji na utumbuaji wa majipu katika maeneo yenye ubadhirifu wa fedha, rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

“Natarajia tutafanya kazi kwa weledi na si nguvu, kwa mfano taarifa zilizotolewa katika maeneo ya bandarini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), siye ndio tulitakiwa tuziwasilishe juu (ngazi ya Rais). Naomba tusisubiri kuletewa,” alisisitiza.

Aliwataka watumishi hao kujiepusha kuwa watuhumiwa wa rushwa.“Jamani hii ni mbaya kwetu Polisi akituhumiwa ujambazi ni mbaya sana, lakini ofisa wa Takukuru akituhumiwa rushwa ni dhambi kubwa. Sisi tuwe watu wa mwisho kutuhumiwa kwa rushwa."

Aliwataka watumishi hao kuelekeza nguvu zao katika kuhakikisha wanaisaidia Serikali kwenye eneo la upotevu wa fedha kwa kufuatilia matumizi na miradi ya maendeleo na fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri na kwenye manunuzi ya umma.

Alisema katika utekelezaji wa jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa nchini kwa mwaka 2014/15 taasisi hiyo ilipokea malalamiko 4,675. Ilifanyia uchunguzi na kukamilisha majalada 667, kupeleka kwa DPP majalada 278, walirejeshewa majalada 172 yenye vibali vya kufungua mashtaka na kufungua kesi mpya 314 nchini kote.

Aidha alisema taasisi hiyo ilishinda kesi 132 mahakamani na washitakiwa walihukumiwa vifungo mbalimbali ikiwemo faini. Ziliokolewa Sh bilioni saba zilizokuwa ziingie kwenye mifuko ya wabadhirifu wachache.

Ndani ya siku 100 za Rais Magufuli madarakani taasisi hiyo ilipokea malalamiko 411 kutoka kwa wananchi, imefungua mafaili 146 ya uchunguzi. Imepeleka kwa DPP mafaili 103, mafaili 65 yenye kibali cha DPP yamerejeshwa kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka, jumla ya kesi 72 mpya zimefunguliwa mahakamani na imeshinda kesi 40 na kushindwa kesi 52.

“Ndani ya siku 100 tumefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 11 akiwemo Mtendaji Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) Kipallo Kisamfu,” alisisitiza.

No comments: