Watu 7 Wafikishwa Mahakamani Kwa Kuvunja Ofisi Ya TRA Makao Makuu Na Kuiba Kompyuta - LEKULE

Breaking

13 Feb 2016

Watu 7 Wafikishwa Mahakamani Kwa Kuvunja Ofisi Ya TRA Makao Makuu Na Kuiba Kompyuta


Watu saba, wakiwamo walinzi wawili wa Suma JKT, wamefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu mashtaka matatu ya kuvunja ofisi ya Makao Makuu ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na kuiba kompyuta na runinga.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba kompyuta aina ya Dell na televisheni moja aina ya Samsung vyenye thamani ya Sh4.2 milioni mali ya TRA.

Mwendesha mashtaka wa Serikali, Hilda Kato aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Joseph Kaitila (24) na Hussein Komba (25) ambao ni walinzi wa Suma JKT, ambalo ni shirika la uzalishaji mali la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). 

Wengine ni Iman Litonto, ambaye ni mfanyabiashara Rajabu Libila (33), Vedasto Mkude (56), mkazi wa Yombo Vituka na madereva, Omary Dikachite (30) na Jumanne Maulid (36).

Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo, Wakili Kato alidai katika shtaka la kwanza, Januari 19 mwaka huu washtakiwa kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa na shtaka la pili washtakiwa hao walivunja ofisi ya Makao ya TRA iliyopo Mtaa wa Sokoine Drive Inn na la tatu ni kuiba vifaa hivyo.

Washitakiwa hao walikana mashtaka hayo na Hakimu Mkazi Flora Mjaya aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 25.

Washtakiwa sita walirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. 

No comments: