Washikiliwa kwa Kumtorosha Mtuhumiwa Gerezani - LEKULE

Breaking

18 Feb 2016

Washikiliwa kwa Kumtorosha Mtuhumiwa Gerezani



Mwanasheria wa Serikali Mkoa wa Katavi pamoja na askari magereza wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo kwa tuhuza za kula njama na kisha kumtorosha kwa siku 124 mtuhumiwa wa kesi ya kujaribu kumuua mlemavu wa ngozi (Albino) baada ya kupokea rushwa ya jumla ya Sh3 milioni.

Tukio la kutoroshwa kwa mtuhumiwa huyo linadaiwa kufanyika Oktoba 12 mwaka jana, baada ya kupokea fedha kiasi hicho ambapo Mwanasheria wa serikali mkoani Katavi, Falhati Seif Khatibu(45) alipokea kiasi cha Sh2 milioni na askari Magareza A.287 S/SGT- John Masagula(50) pamoja na A. 5385 SGT Deogratius Katani(50) wakigawana kiasi cha Sh milioni moja.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kulifanikiwa kutokana na taarifa za siri kutoka kwa raia wema ambao walidai kuwa kuna mtuhumiwa aliyekuwa anashikiliwa ametoroka kutoka katika gereza la mahabusu la Mpanda lililopo mkoani humo.

Alisema baada ya taarifa hizo ndipo uchunguzi ulipofanyika Januari 19 mwaka huu, na kubaini kuwa mtuhumiwa Alex Manyanza(27) ambaye alikuwa anashikiliwa kwa tuhuza za kujaribu kumuua kwa kumkata kiganja cha mkono mlemavu wa ngozi Limi Luchoma(30), mwanzoni mwa mwaka na kufunguliwa shitaka namba MTO/IR/76/2015 alikuwa ametoroka mahabusu.

Baada ya upelelezi ilibainika kuwa ndugu wa mtuhumiwa huyo ndio waliotekeleza mpango huo na kisha kumtorosha mtuhumiwa na kwenda kumficha katika kijiji cha Kipande kilichopo mkoani Rukwa, na ndipo walipompa fedha hizo mwanasheria mkuu wa serikali ili amuondelee shitaka linalomkabili mtuhumiwa huyo baada ya kufanikiwa kutoroka gerezani.

Alisema mtuhumiwa ni mzoefu kwa vitendo vya kutoroka gerezani kwani kabla ya kufanya tukio hilo alikuwa ametoroka katika gereza la Kalila Nkulunkulu lililopo mkoani humo, ambapo alikuwa anatumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya mahakama kumtia hatiani kwa kosa la wizi wa mifugo.

No comments: