Wasanii Waidai Mamilioni Ya Pesa IKULU....Deni hilo Liliachwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete - LEKULE

Breaking

25 Feb 2016

Wasanii Waidai Mamilioni Ya Pesa IKULU....Deni hilo Liliachwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete



Ikulu imeahidi kufanyia kazi madai ya Chama cha Wasanii Wachoraji Tanzania (Chawata), ambayo waliyawasilisha jana, kikilalamikia ofisi hiyo katika awamu ya nne iliyokuwa chini ya Rais Jakaya Kikwete, kuwacheleweshea malipo yao ya Sh. milioni 53.6.

Kwa mujibu wa taarifa ya Chawata kwa vyombo vya habari jana, fedha hizo zimetokana na kazi za sanaa ambazo zilichukuliwa na serikali ya awamu ya nne kutoka kwa wafanyabiashara wa eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam na kupelekwa Ikulu.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, alithibitisha kuwapo na madai hayo na kusema kuwa yatafanyiwa kazi ndani ya wiki moja kuanzia jana.

“Ni kweli Ikulu inadaiwa, lakini ni deni la awamu ya nne, kwa hiyo tumewaomba kuwakamilishia madai yao ndani ya wiki moja, baada ya kufanya uhakiki ili kujiridhisha,” alisema Msigwa.

Awali, Katibu wa Chawata, Cuthbert Semgoja alisema waliahidiwa kulipwa fedha hizo kabla ya uchaguzi mkuu mwaka jana lakini hadi sasa hawajalipwa.

"Tuliuza kazi zetu Ikulu kwa makubaliano ya kulipwa baadaye tangu Agosti mwaka jana, hadi leo hii (jana) bado hatujaweza kupatiwa pesa zetu," alisema na kuongeza:

“Mchakato wa kazi zetu ulianza mwishoni mwa mwezi wa nane kwa kamati husika, kupitia katika maeneo ya wasanii, ili kuweza kufanya chaguzi ya sanaa wanazohitaji. Walijiridhisha kwa kuchukua baadhi ya sanaa kutoka kwa wanakikundi kwa ahadi ya kufanya malipo mara moja kabla ya uchaguzi mkuu lakini hadi sasa bado malipo hayo,” alisema Semgoja.

Alisema baada ya chama kuona muda wa malipo unakwisha, walichukua jukumu la kupiga simu kwa mhusika ambaye walikuwa wakifanya naye biashara hiyo kwa niaba ya Ikulu, lakini jibu lake lilikuwa `malipo yenu yanaandaliwa.'

“Baada ya mwezi mmoja kufanya biashara hiyo, tulianza kumpigia simu mtu mmoja ambaye ndiye alikuwa anahusika na sisi tangu mwanzo wa biashara yetu hadi mwisho, lakini majibu tunayopewa ni kusubiri tu, tumechoka sasa,” alisema.

Alisema mawasiliano waliyokuwa wanafanya na mtu kutoka Ikulu ambaye alijitambulisha (jina tunalo), ndiye aliyekuwa akiwapa majibu hayo kuhusu madai yao.

Aliongeza kuwa kulingana na ahadi waliyopewa kulipwa kabla ya uchaguzi mkuu na mlolongo wa ahadi zinazojirudia, walianza kufanya mawasiliano wao kwa wao ili  kufahamu nini kinachoendelea kuhusu malipo yao na kugundua kuwa kuna tatizo.

“Ilifika hatua simu zetu hazipokelewi, kila tunapopiga mhusika hapokei simu zetu, ndipo hapo tulipohisi kuna mchezo unaendelea kati ya mtu huyo na chama chetu,” alisema.

No comments: