UNFPA yaitaja Tanzania kuwa moja ya nchi tatu zinazoongoza kwa ndoa za utotoni - LEKULE

Breaking

29 Feb 2016

UNFPA yaitaja Tanzania kuwa moja ya nchi tatu zinazoongoza kwa ndoa za utotoni


Picture1
Imeelezwa kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambayo bado inakabiliwa na changamoto ya ndoa za utotoni ambazo husabishwa na mila potufu, elimu duni na umaskini unaopelekea wazazi kuwa na tamaa za kupata mali ili waweze kukidhi haja zao pamoja na sheria kandamizi.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la watu duniani (UNFPA) imeonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya tatu inayoongoza kwa ndoa za utotoni duniani kwa kuwa na kiwango cha juu ukilinganisha na nchi zingine duniani.
Akielezea kuhusu ripoti hiyo, ofisini kwake,Mwanasheria wa TAMWA Bi. Loyce Gondwe alisema kuwa mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni Shinyanga, Tabora, Mara, Dodoma, Lindi, Mbeya, Morogoro, Singida, Manyara, Mtwara, Pwani, Arusha, Kilimanjaro, Kigoma, Dar Es salaam na Iringa.
Bi.Gondwe, alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 13 kimeruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya mahakama na miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi na mtoto wa kiume aliyefikisha umri wa miaka 18 anaweza kuoa.
Ameendelea kusema kuwa licha ya kuwepo kwa sheria ya mtoto ya mwaka 2009, inayotafsiri kwamba mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18 bado sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inawaruhusu watoto wa kike chini ya miaka 18 kuolewa na hivyo sheria ya ndoa kukinzana na sheria zingine.
Hata hivyo, alisema licha ya Tanzania kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayopinga na kuzuia ndoa za utotoni, kama Mkataba wa Haki za watoto wa mwaka 1989, ambao unamtafsiri mtoto kama yeyote mwenye umri chini ya miaka 18 na Tamko la Haki za Binadamu ulimwenguni la mwaka 1948, Ibara ya 16(2) bado tatizo la ndoa za utotoni limeendelea kuwepo.
Naye mratibu wa kituo cha usuluhishi TAMWA, Bi. Gladness Munuo alisema kuwa ndoa za utotoni zina madhara mengi kwa mtoto ikiwemo kumyima haki yake ya msingi ya kupata elimu na hivyo kumpotezea ndoto zake za kimaisha.
Bi. Munuo alisema Ndoa za utotoni zinaweza kuleta madhara ya kiafya kwa mtoto ikiwemo magonjwa ya fistula, ulemavu wa kudumu kwa sababu viungo haviko tayari kushiriki tendo la ndoa na kushika mimba.
Aliendelea kusema kuwa mtoto mdogo anapoingia kwenye ndoa anakumbana na changamoto kubwa zingine za ndoa, kwa mfano migogoro ya ndoa kama vile kupigwa, kufukuzwa, ulevi, utelekezwaji ambavyo hupelekea madhara makubwa kwa mtoto katika maisha yake.
Hata hivyo alitoa wito kwa serikali, jamii, watu binafsi na taasisi mbalimbali kulinda haki za watoto ikiwemo kuchukua hatua ya kutoa taarifa sehemu husika ili suala hilo liweze kuchukuliwa hatua na kutatuliwa.

No comments: