TRA Yaendelea Kuikaba Koo StarTimes - LEKULE

Breaking

3 Feb 2016

TRA Yaendelea Kuikaba Koo StarTimes


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema Kampuni ya StarTimes inayouza ving’amuzi kwa ajili ya ‘chaneli’ mbalimbali za televisheni, ikiwamo Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) inafanya biashara ya simu kupitia mgongo wa mtu.

Hilo limebainika katika uchunguzi unaofanywa na TRA dhidi ya kampuni hiyo, kufuatia maboksi 294 yaliyokamatwa yakiwa na simu 2,744 na vifaa vyake ndani ya ghala lake mwezi uliopita.

Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipakodi, Richard Kayombo alisema uchunguzi unaoendelea kufanywa umebaini kuwa maboksi hayo yalikuwa ya StarTimes, tofauti na taarifa za nyaraka za mizigo zilivyokuwa zikieleza kuwa mizigo ni ya mtu mwingine.

“Tulifuatilia tukabaini hii biashara ambayo wanaifanya Startimes wanamtumia mtu mwingine kama sehemu ya kukwepa kodi, kwani nyaraka zilionyesha mzigo ni wa mtu mwingine, lakini katika kuchunguza tumebaini ni wa StarTimes,” alisema Kayombo.

Alisema wanaendelea na uchunguzi zaidi ili kujua kama biashara hiyo inayotumia jina la mtu imekuwa ikifanywa kwa muda gani, lakini pia wanaendelea kufanya utaratibu wa kampuni hiyo kulipa kodi ya mizigo hiyo.

“Bado tunafanya taratibu za namna ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ambayo ilitakiwa ya Sh118 milioni,” alisema.

Mwenyekiti wa bodi ya StarTimes, Clement Mshana alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema maswali hayo aulizwe Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Lanfang Liao huku akisisitiza hana taarifa za kina kuhusu ripoti hiyo.

“Mwambie akufahamishe zaidi huyo ndiye mtendaji mkuu wa kampuni. Hata hivyo hiyo stori inayomkariri mtu wa TRA sijaisoma hivyo sina taarifa za kina juu ya alichoeleza TRA,” alisema.

Hata hivyo, alipoombwa namba yake ya simu hakuwa tayari kutoa, badala yake alituma ujumbe wa maneno uliosema kuwa “nimemwambia ofisa uhusiano atakupigia”.

No comments: