Toka Bungeni: Hatimaye Bunge Laanza Kujadili Mpango wa Maendeleo Uliokwama Kuwasilishwa Bungeni Wiki Iliyopita - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Monday, 1 February 2016

Toka Bungeni: Hatimaye Bunge Laanza Kujadili Mpango wa Maendeleo Uliokwama Kuwasilishwa Bungeni Wiki Iliyopita

Hatimaye leo Bunge limeanza kujadili mpango wa maendeleo ya mwaka 2016/2017, baada ya bunge hilo kutengua kanuni ili kupitisha mpango huo ambao ulikataliwa wa baadhi ya wabunge wiki iliyopita.

Akiwasilisha Mpango huo Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema mpango huo umeweka kipaumbe cha kuanzisha na kuendeleza viwanda vinavyotokana na rasilimali zinazopatikana nchini pamoja na viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazotumiwa na watu wengi.

Dkt. Mpango amesema katika mapango huo serikali imepanga kukusanya shilingi trilioni 14.16 kutokana na mapato ya kodi katika mwaka wa fedha 2016/2017 ambayo ni ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na mapato ya kodi ya fedha yaliyokusanywa mwaka uliopita.

Aidha katika mwaka wa fedha 2016/2017, serikali imepanga kutumia shilingi trilioni 22 .99 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo ambapo kati ya hizo trilioni 16.80 itakuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 6.18 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Amesema kati ya trilion 16.80 za matumizi ya kawaida, shilingi trilion 6.65 zitakuwa ni kwa ajili ya mishahara.

Aidha amesema kuwa kati ya trilion 6.18 za miradi ya maendeleo, takriban trilion 4 sawa na asilimia 77.8 zitakuwa ni fedha za ndani.

Bunge litakaa kama kamati kujadili na kutoka mapendekezo kwa ajili ya kuboresha mpango huo kwa  siku tano kuanzia leo.


Mpango huo uliingia dosari wiki iliyopita baada ya wabunge wa upinzani kukataa kuujadili kwa madai kuwa serikali ilikiuka kanuni na taratibu za kuuwasilisha bungeni.
Post a Comment