Serikali Yajieleza Bungeni Kinachosababisha Umeme Ukatike Mara Kwa Mara - LEKULE

Breaking

5 Feb 2016

Serikali Yajieleza Bungeni Kinachosababisha Umeme Ukatike Mara Kwa Mara



Serikali  imesema tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini linatokana na uchakavu na kuzidiwa kwa vituo vya kupoza umeme na miundombinu ya usafirishaji na usambazaji nishati hiyo.

Katika kukabiliana na tatizo hilo Tanesco inachukua hatua za kujenga mifumo ya njia kubwa za umeme wa msongo wa kilovoti 400 (Iringa- Dodoma-Singida-Shinyanga), gridi ya Kaskazini Mashariki (Dar es Salaam, Chalinze,Tanga –Arusha), ya Kaskazini Magharibi (Geita- Kagera –Katavi- Kigoma- Rukwa na Mbeya) na Makambako- Songea wa kilovoti 220.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani wakati akijibu swali la Mbunge wa Magu, Boniventure Kiswaga (CCM). 

Kiswaga alitaka kufahamu serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la kukatika katika kwa umeme.

Pia mbunge huyo alitaka kufahamu, Je serikali itakamilisha lini kupeleka umeme katika vijiji vya jimbo hilo ikizingatiwa mpaka sasa ni asilimia 20 tu ya vijiji ndiyo vina umeme. 

Kalemani akijibu swali hilo, alisema tatizo la kukatika kwa umeme linatokana na uchakavu na kuzidiwa kwa miundombinu ya kupoza umeme pamoja na matukio ya kulipuka kwa transfoma yanayosababishwa na radi hasa kipindi cha mvua pamoja na wizi wa mafuta ya transfoma unaofanywa na wananchi wasio waaminifu.

Alisema Tanesco inakamilisha upanuzi wa usambazaji wa umeme katika majiji makubwa ya Arusha, Dar es Salaam, na Mwanza ambapo kazi hizo zitahusisha ujenzi wa njia mpya za umeme na kupanua vituo vya kupoza umeme.

“Kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA mkoani Kilimanjaro kumeimarisha upatikanaji wa umeme maeneo ya Mirerani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA),” alisema Kalemani.

Pia vituo vya kupoza umeme katika jiji la Dar es Salaam vya Gongo la Mboto, Kipawa, Mbagala, na Kurasini vitaunganishwa kwa njia ya sakiti mzunguko kutoka Ubungo na Kinyerezi kuanzia Machi mwaka huu.

No comments: