Serikali yabaini wizi wa takribani Milioni 700 ATCL....Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika Hilo Bw.Steven Kasubi Asimamishwa Kazi Kupisha Uchunguzi - LEKULE

Breaking

10 Feb 2016

Serikali yabaini wizi wa takribani Milioni 700 ATCL....Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika Hilo Bw.Steven Kasubi Asimamishwa Kazi Kupisha Uchunguzi



Serikali imebaini wizi wa  takribani  shilingi Milioni 700 katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kupitia kampuni ya Wakala wa ukatishaji tiketi ya Salama World Travel iliyopo visiwa vya Komoro.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ,Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa ameeleza kuwa  wizi huo umefanywa kwa kushirikiana na wafanyakazi wa shirika hilo.

“Kufuatia upotevu huo Serikali  imechukua hatua thabiti ikiwemo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa ATCL Bw.Steven Kasubi ili kupisha uchunguzi utakaofanywa na kikosi  cha polisi  kitengo cha usalama mtandaoni  ili kubaini mtandao mzima uliohusika  ” alisema Prof.Mbarawa.

Aidha aliongeza kuwa kwa utaratibu wa kawaida wa  shirika hilo wakala anapewa ruhusa ya  kuuza tiketi za ndege kuanzia kiasi cha shilingi milioni 15 tu na pale anapomaliza mauzo anarudisha fedha kwa shirika na baadaye kupewa ruhusa tena.

Prof.Mbarawa anasema kwa sasa wameanza na shirika la Ndege la Tanzania kwa kwa lengo la kulifufua kwa kununua ndege mpya na kuwa na wafanyakazi wachapakazi na waadilifu.

“Siku mbili zilizopita nilifanikiwa kukutana na menejimenti ya ATCL na kubaini mapungufu mengi na hivyo kuamua kuyafanyia kazi kwa kuhakikisha shirika hii linarudi kutenda kazi kwa udhabiti kwa kuwashughuikia wale wote wanaoenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma” alisema Prof.Mbarawa.

Vilevile aliongeza kuwa Serikali imemuagiza  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kufanya uchunguzi kwa mawakala wengine wote wa Shirika hilo kubaini kama fedha za uuzaji wa tiketi hizo zinarudishwa kama inavyotakiwa.

Prof.Mbarawa ametoa wito kwa wananchi kuachana na wizi kwa  njia ya mtandao kwa kuwa sheria ya mtandao iliyoanzishwa mwaka jana inatumika katika kuhakikisha kuwa watuhumiwa wanafikishwa katika mkondo wa sheria na kuchukuliwa hatua stahiki.

No comments: