Polisi wapigana na Chupa za Bia Baa - LEKULE

Breaking

15 Feb 2016

Polisi wapigana na Chupa za Bia Baa


Kigogo mmoja katika Kituo cha Polisi Kachwamba, wilayani Chato, mkoani Geita, anadaiwa kumjeruhi vibaya askari mwenzake baada ya kumshambulia kwa chupa ya bia wakiwa kwenye baa.

Kituo hicho cha polisi kipo kata ya Kachwamba, nje ya makao makuu ya wilaya ya Chato, lakini wakati tukio hilo  likifanyika kigogo huyo alikuwa Chato mjini.

Askari aliyejeruhiwa, PC Deus Sigera wa kitengo cha upelelezi katika kituo cha polisi Chato, amedaiwa kujeruhiwa kwenye paji la uso pamoja na shavuni na eneo la mdomo aliumia vibaya.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi wakati polisi hao wakipata kinywaji kwenye baa moja iliyopo Chato mjini.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo na aliyeamulia ugomvi huo kabla ya kutakiwa kwenda kutoa maelezo polisi, Sunday Baregu, ambaye pia ni ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Chato, amesema  kuwa wawili hao walianza kwa kujibizana kwa maneno makali.

Alisema baada ya majibizano hayo, kigogo huyo wa polisi alichukua chupa ya kinywaji alichokuwa akikitumia kisha kumshambulia mwenzake usoni na shavuni kabla ya kusaidiana na wasamaria wema kuamua ugomvi huo na kumwahisha hospitali kwa matibabu.

“Ni kweli niliamulia ugomvi huo na baadaye kuongozana na aliyejeruhiwa kwenda kutoa maelezo polisi na kupewa PF3 (hati ya matibabu), lakini kwa taarifa zaidi labda liulize Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita kwa kuwa mimi siwezi kulizungumzia hilo,” alisema.

Hata hivyo, habari kutoka vyanzo mbalimbali zinaarifu kuwa  baada ya tukio hilo kigogo huyo alikamatwa na kuswekwa mahabusu wakati mwenzake, PC Deus akiendelea kupata matibabu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Chato.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Latson Mwabulambo, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema bado hajapokea taarifa rasmi kutoka kwa wasaidizi wake na kwamba wanaendelea na upelekezi wa tukio hilo.

Aidha, alidai kuwa hakuwa ofisini kwake kwani alikwenda kata ya Manyovu Runzewe kwa shughuli za kikazi.

No comments: