Nape Nauye Aanika Siri Ya Mafanikio Ya CCM Kuendelea Kushika Dola - LEKULE

Breaking

5 Feb 2016

Nape Nauye Aanika Siri Ya Mafanikio Ya CCM Kuendelea Kushika Dola


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kushika dola licha ya upinzani mkali kutoka vyama vingine vya siasa hasa vile vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwake, yanaandika historia nyingine ya chama hicho tangu kuanzishwa kwake Februari 5, 1977.

Chini ya Baba wa Taifa Mwalimu, Julius Nyerere chama hicho ambacho ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika kikitanguliwa na ANC cha Afrika Kusini, kinajivunia mambo mengi yaliyokifanya kudumu mpaka sasa wakati vyama vikongwe vya nchi nyingine kama Zambia (UNIP), Kenya (Kanu) na Malawi vikiwa vimeshaondolewa madarakani.

Nape ataja siri ya mafanikio 
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye anasema mfumo wa chama hicho kujiimarisha kimtandao kuanzia ngazi ya shina kwa maana ya balozi wa nyumba kumi mpaka taifa umekifanya kiendelee kuwa kimbilio la wananchi wengi hadi kufikia kupata wanachama zaidi ya milioni sita, kutoka wanachama wachache waliokuwapo miaka iliyopita.

“Chama chetu kimeendelea kuwa na sura ya kitaifa, kalenda inayojulikana ambayo imekuwa ikiruhusu chaguzi kila baada ya miaka mitano na kuifanya Tanzania kuwa nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia,” anasema.

Yapo baadhi ya mambo ambayo chama hicho kinajivunia kwa miaka 39 tangu kizaliwe. 

Kuendelea kushika dola 
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Patrick Myovela anasema mafanikio ya chama hicho ni pamoja na ushindi kwenye chaguzi mbalimbali zilizowawezesha kuendelea kushika dola.

“Tumepata ushindi uliotuwezesha kushika dola katika chaguzi kuu zilizofanyika zaidi ya mara sita. Tumeishi kwenye shabaha ya chama chetu ile inayotaka kuendelea kuwa madarakani, tukiunda na kusimamia Serikali,” anasema.

Myovela ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema, CCM bado inaaminiwa na Watanzania wengi ndiyo maana wameendelea kukipa kura na kukiwezesha kuunda Serikali. Hiyo imetokana na imani ya wananchi juu ya chama hicho.

Nape anasema mara zote CCM imekuwa ikichagua mgombea urais atakayeweza kushika bendera ya chama hicho kwa umakini zaidi kwa kuzingatia matakwa ya wananchi kwa wakati husika.

Uongozi wa kupokezana 
Kati ya vitu ambavyo vimeiletea sifa kubwa Tanzania ni pamoja na kuwa na uongozi wa kupokezana madaraka. 

Wakati nchi nyingine ikiwamo Uganda, Burundi na Zimbabwe zikivurugana kutokana na vyama vinavyotawala kushindwa kuenzi dhana ya kupokezana, tayari Tanzania imeshapitia awamu tano za uongozi na kila awamu ikiongozwa na rais tofauti.

“Baada ya kuongoza miaka 23, Mwalimu Nyerere aliamua kung’atuka akimuachia Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye aliingia kwa kupigiwa kura licha ya kuwapo kwa mfumo wa chama kimoja,”anasema Nape.

Anasema uongozi huo wa nchi  kupokezana ulimfanya Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa kushikilia usukani akimpokea Mwinyi hadi mwaka 2005 alipomkabidhi Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na mwaka jana Rais John Magufuli.

Myovela anasema ni dhahiri taswira nzuri ya uongozi wa nchi inatokana na uimara wa chama kilichopo madarakani. 

Demokrasia ya vyama vingi
Licha ya kuwapo kwa mabadiliko ya kidemokrasia hususan mfumo wa vyama vingi ulioasisiwa na CCM yenyewe mwaka 1992, chama hicho kimeendelea kushamiri huku kikishinda chaguzi zote kuu na zile za mitaa.

Nape anasema wakati CCM iliamua kuasisi mfumo huo, wananchi wengi walitamani kiendelee kuwa peke yake.

“Kumbuka kwamba wakati wa kura ya maoni ya kuendelea kuwa na mfumo wa chama kimoja au kuwa na vyama vingi vya siasa, Watanzania wengi walipendekeza kuendelea kuwapo kwa chama kimoja, lakini kutokana na demokrasia, CCM iliamua kuruhusu mfumo wa vyama vingi kuanza nchini,” anasema.

Mpaka sasa Tanzania ina vyama vya siasa zaidi ya 20 vilivyosajiliwa, vingi vikiwa vimefanikiwa kushiriki katika chaguzi mbalimbali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Enock Ugulumu ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa anasema kama kingeendelea kuwa na mgombea mmoja kila kinapoingia madarakani, uhakika wa kuwapo mpaka leo usingekuwapo.

“Mfumo wa kubadilishana uongozi ndiyo siri kubwa ya ushindi wa CCM, hatung’ang’anii madaraka kwa sababu Katiba ya CCM imeruhusu demokrasia tangu ndani, mpaka nje kwenye umma.

"Vinginevyo Mwenyekiti wa CCM Taifa asingetaka kutoka kwa miaka yote, angebaki kuwa yuleyule,” anasema.

Vipo vyama ambavyo vimeshindwa kuzingatia mfumo wa kubadilishana madaraka kwa kuwa na viongozi wale wale tangu kuanzishwa kwake.

 Katiba Mpya 
Mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya unaonyesha namna ambavyo CCM ilivyofanikiwa kupokea na kufanyia kazi ushauri na mapendekezo yanayotolewa na wananchi kutoka katika kada zote.

Nape anasema CCM inajivunia kuwa na mchakato huo hata kama haujafikia mwisho. Anasema uwepo wa rasimu iliyopita kwenye Bunge la Katiba kunaifanya CCM ionekane inasikiliza maoni ya Watanzania na kuyatumia inapowezekana.

“Ni chama kilichodumu kwa muda mrefu, kinajivunia kuwa kisikivu na kutimiza mahitaji ya Watanzania.” Anasema bila nia njema ya kukubali mchakato huo uwepo, usingeanzishwa na kufikia hatua ya kura za maoni ilipo sasa.

Kulinda na kudumisha amani nchini
Nape anasema katika tunu za taifa mbazo CCM inajivunia kuziendeleza tangu uhuru kuwa ni kulinda na kudumisha amani.

Katika miaka yote, CCM imekuwa ikiagiza na kusimamia kuhakikisha Serikali inalinda na kudumisha misingi imara ya amani iliyoasisiwa na waanzilishi wa taifa.

Hata hivyo, anasema CCM imeshiriki katika harakati za kutafuta ukombozi wa nchi majirani ili kujihakikishia usalama ndani na  nje ya nchi 

Uhuru, umoja na mshikamano .
Myovela anasema ni ukweli usiopingika kuwa umoja na mshikamano uliopo nchini unatokana na usimamizi mzuri wa Serikali inayoundwa na chama hicho.

Anasema kutokuwa na ubaguzi wa aina yoyote ile ikiwamo udini, ukabila, rangi wala ukanda unatokana na misingi mizuri iliyowekwa na chama hicho tangu kuundwa kwake. 

Nape anasema kitendo cha kuwa na ilani za uchaguzi zinazogusa maisha ya watu wa kila kada, kimeisaidia Serikali kutimiza wajibu wake.

“Kila mwaka wa uchaguzi, CCM imekuwa ikiisimamia Serikali katika kutimiza majukumu yake kupitia ilani ya uchaguzi. Ukisoma ilani zote utagundua CCM haikurupuki, inafanya mambo yake kwa umakini mkubwa. Hili tunajivunia,” anasema Nape.

Anasema msingi wa utawala bora lazima uendane na kile ambacho chama kingependa wananchi wake wafanyiwe kwa kuiagiza Serikali kupitia ilani yake.

Anasema viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa taarifa ya utekelezaji wao wa majukumu kwa chama ili kipate nafasi ya kukosoa na kusonga mbele.

Utawala bora 
Nape anasema Watanzania wameshuhudia uanzishwaji wa mikoa, wilaya, kata na vijiji vipya ili kuwasogezea huduma karibu. 

Maazimio 

Anasema kuna maazimio mbalimbali likiwamo Azimio la Mtowisa lililotaka kila kaya kujitosheleza kwa chakula na Azimio la Zanzibar lililofungua Demokrasia ya ndani ya CCM, haya yote yamechangia katika mafanikio ya CCM.

No comments: