Mwenyekiti Wa Kijij Chadema Akataliwa - LEKULE

Breaking

5 Feb 2016

Mwenyekiti Wa Kijij Chadema Akataliwa



Wakazi wa Kitongoji cha Misungwi D, Kijiji cha Misungwi wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza wamemkataa Mwenyekiti wao, Raphael Kimoka (Chadema) kwa tuhuma za kutowasomea taarifa za mapato na matumizi ya fedha tangu achaguliwe.

Walitoa msimamo huo kwenye mkutano mkuu wa kitongoji uliofanyika juzi.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Misungwi, Amos Seko alisema wakazi hao wamekuwa wakishindwa kufanya shughuli za maendeleo, huku wakiendelea na vikao na kuweka maazimio ya kutokuwa na imani na mwenyekiti wao.

“Leo ni kikao cha mwisho kuhusiana na malalamiko yenu dhidi ya mwenyekiti mliyoyaleta tangu Oktoba 27, mwaka jana. Mtaamua wenyewe hapa ama aendelee au la,” alisema Seko.

Seko alisoma tuhuma nyingine dhidi ya mwenyekiti zilizopelekwa kwake na wakazi hao kuwa ni kutosimamia majukumu yake vizuri, kubagua wananchi wakati wa kutoa huduma, kutohudhuria vikao vya kitongoji vya maafa na kutetea uhalifu.

Mwakilishi wa mkuu wa wilaya ambaye ni Ofisa Tarafa wa Misungwi, Peter Marco alisema tuhuma dhidi ya mwenyekiti huyo ziliwasilishwa kwenye kikao cha halmashauri ya kijiji cha Novemba 11, mwaka jana, Alisema kiongozi huyo alipewa nafasi ya kujitetea, lakini hakufanya hivyo badala yake alitoka nje ya kikao.

Kimoka alipopewa nafasi ya kujitetea, alidai kuwa mkutano huo umeandaliwa kisiasa, hivyo hautambui kwa sababu wengi wao ni wanachama wa CCM.

“Waliohudhuria hawakunitendea haki, sikubaliani nao,” alisema.

Aliongeza kuwa, kwa muda mrefu alijua kulikuwa na mpango wa kutaka kumuondoa madarakani wenye msukumo wa kisiasa.

No comments: