Mkuu Mpya Wa Chuo Kikuu Cha Dar (UDSM) Rais mstaafu Jakaya Kikwete Atembelea Chuo Hicho Na Kujionea Hali Halisi Ilivyo - LEKULE

Breaking

10 Feb 2016

Mkuu Mpya Wa Chuo Kikuu Cha Dar (UDSM) Rais mstaafu Jakaya Kikwete Atembelea Chuo Hicho Na Kujionea Hali Halisi Ilivyo



MKUU mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ametembelea chuo hicho kujifunza na kujionea hali halisi ilivyo, kabla ya kukabidhiwa rasmi wadhifa huo.

Kikwete aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, ameteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo, baada ya kufariki kwa Balozi Fulgence Kazaura mwaka 2013.

 Akiwa chuoni hapo majira ya mchana, Kikwete alitembelea Chuo cha Uhandisi, Jengo jipya la Sayansi, kumbi za mihadhara za Yombo na eneo ambalo itajengwa maktaba mpya ya kisasa.

Akiwa katika Ukumbi wa Yombo, aliwaambia wanafunzi kuwa Rais John Magufuli amempa kazi ya kuwa mkuu wa chuo, hivyo amefika hapo kujionea hali halisi kabla ya kukaa na viongozi kutengeneza chuo hicho kiwe bora zaidi.

Akiondoka katika eneo la ukumbi huo, baadhi ya wanafunzi walimfuata na kumweleza kuwa zaidi ya miezi miwili hawajapewa fedha za kujikimu, hivyo aliwaahidi kuwasaidia kwa kulisemea sehemu husika.

Baada ya ziara hiyo, Kikwete alikutana na watendaji mbalimbali wa chuo hicho na kuwaeleza kuwa ujio huo umempa kukifahamu chuo hicho kwa sehemu. “Nimefurahi fursa hii ya kutembea leo (jana) kabla ya siku rasmi ya kukabidhiwa uongozi wa chuo.

"Bado natamani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiwe bora kuliko vyote nchini. Sina maana vingine vitakuwa duni, hapana. Ila kiwe ni chuo kinachotoa viongozi. Mtu akitaka kiongozi aanzie kumtafuta kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akikosa ndio aende chuo kingine.

"Na hivyo vyuo vingine watafute maeneo ambayo watayakomalia ili nao wafuatwe,” alisema Kikwete ambaye alisoma hapo katika miaka ya 1970. 

Alisema amesikia kilio cha wanafunzi hao baada ya kumwambia hali ni tete kwa kuwa hawajapata fedha, hivyo japo hajakabidhiwa rasmi nafasi hiyo, ataanza na hilo ili vijana wasome vizuri.

Aliahidi kurudi kabla ya mwezi huu kuisha ili akutane na viongozi mbalimbali, lengo ni kukielewa vizuri kabla ya kukabidhiwa rasmi.

No comments: