Maofisa wa Wizara ya Afya Wahama Muhimbili Kutekeleza Agizo La Rais Magufuli - LEKULE

Breaking

15 Feb 2016

Maofisa wa Wizara ya Afya Wahama Muhimbili Kutekeleza Agizo La Rais Magufuli



AGIZO la Rais John Magufuli la kuibadilisha jengo la maofisa wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto lililopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, limetelekezwa baada ya jana maofisa hao kuondoa vifaa vyao.
 
Tangu jana asubuhi maofisa wa wizara hiyo Kitengo cha Afya ya Uzazi na Watoto wakiongozwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya walikuwa wakiondoa vifaa na kupakia kwenye magari.
 
“Ikifika jioni vifaa vyote vitakuwa vimeondolea ndani na katika eneo hili,” alisema Ulisubisya na kueleza kuwa ofisi hizo zitahamia wizarani Barabara ya Sokoine jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza baada ya kukagua uondokaji wa maofisa hayo, Waziri Ummy Mwalimu alisema agizo la Rais limetekelezwa na kusisitiza kuwa hakuna mgonjwa atakayelala chini.
 
Alisema pamoja na kuwa kazi ya kulipangia matumizi jengo hilo ni ya uongozi wa Muhimbili, uongozi wake utasimamia kuhakikisha jengo hilo lenye ghorofa tatu linatumika kama wodi katika kupunguza msongamono katika wodi ya wazazi.
 
Mwalimu alisema baada ya kuhamishwa maofisa hao, kinachofuata ni kufanya ukarabati wa kuongeza vyoo na mabafu ili yaendane na viwango vya wodi inavyotakiwa na baadaye kuwekwa vitanda takribani 300.
 
Akitoa maelezo kwa Waziri, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema katika kutatua tatizo hilo kwa muda wameamua kutumia ghorofa ya chini, ambayo ilikuwa ikitumika kama kliniki ya wajawazito na watoto chini ya siku 30 na kuweka vitanda kwa ajili ya wagonjwa 50.
 
“Mpaka leo (jana) tulikuwa na wagonjwa 50 waliokuwa wamelala chini, hivyo tumeamua kutumia eneo lililokuwa likitumiwa kama kliniki kuwa wodi kwasababu ya kuwa na vyoo na mabafu. Baada ya maofisa wa wizara kuondoka, eneo la chini la jengo la ghorofa tatu litatumika kama kliniki,” alisema Profesa Museru.
 
Naye Asha Twalib aliyekuwapo hospitalini hapo kumuona mgonjwa wake, alipongeza juhudi za Rais Magufuli katika kuboresha sekta ya afya nchini.
 
Rais Magufuli ambaye alisimamishwa na akina mama hospitalini hapo na kutembelea wodi ya wazazi wiki iliyopita, alitoa siku mbili kwa maofisa 70 wa wizara Kitengo cha afya ya Uzazi na Mtoto kuhama katika jengo hilo na kuhamishia wazazi ili kila mzazi apate kitanda cha kulala.
 
“Nimeshatoa agizo lile jengo la ofisi la uzazi ndani ya siku mbili wahame...wakiweza wakakae na Waziri (Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto).

 “Ndani ya siku mbili hizo hizo, pawe na vitanda na wale akinamama (wajawazito wanaolala watano kitanda kimoja), wahamishiwe kule,”alisema Rais Magufuli alipozungumza na Taifa juzi kupitia kwa wazee wa Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee akitimiza siku 100 tangu aingie Ikulu ya Magogoni.

No comments: