Mahakama Yashusha Rungu kwa Majangili........Yawapiga Kifungo cha Miaka 20 na Faini ya Milioni 270 - LEKULE

Breaking

1 Feb 2016

Mahakama Yashusha Rungu kwa Majangili........Yawapiga Kifungo cha Miaka 20 na Faini ya Milioni 270


Mahakama ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida, imewahukumu mtu na kaka yake, kutumikia kifungu cha miaka 20 kila mmoja na kulipa fidia ya sh. milioni 270, baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kukutwa na meno ya tembo, silaha na risasi kinyume cha sheria.

Washitakiwa hao ni Nicodem Mchongareli na Festol Mchongareli, ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 13 ya mwaka jana. 
Wanadaiwa kukutwa na meno ya tembo mawili yenye thamani ya sh. milioni 27, bunduki tatu zikiwemo za aina ya Riffle, risasi 25 na maganda yake 15.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Joyce Minde, baada ya upande wa Jamhuri uliokuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Salim Msemo na ule wa utetezi kufunga ushahidi.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Joyce alisema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa jamhuri ulileta mashahidi watano na washitakiwa baada ya kuonekana wana kesi ya kujibu walijitetea wenyewe.

“Mahakama imewaona washitakiwa hao wana hatia baada ya upande wa Jamhuri kuthibitisha mashitaka dhidi yao pasi na kuacha shaka yoyote,” alisema.

Hakimu huyo aliwapa adhabu washitakiwa hao kwa kukutwa na meno ya tembo, kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja na kulipa serikali sh. milioni 270. 
Pia shitaka la pili wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya sh. milioni 333 na makosa mengine kutumilia kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya sh. milioni mbili kwa kila shitaka.


Adhabu za vifungo zinakwenda sambamba, hivyo washitakiwa hao watatumikia kifungo cha miaka 20 kila mmoja

No comments: