Maalim Seif Shariff Hamad Adai Kikwete Ndiye Aliyevuruga Uchaguzi Zanzibar - LEKULE

Breaking

4 Feb 2016

Maalim Seif Shariff Hamad Adai Kikwete Ndiye Aliyevuruga Uchaguzi Zanzibar



Mgombea  urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad amemtuhumu Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kwa kuingilia uchaguzi Zanzibar.

Akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa wilaya na majimbo wa chama hicho uliofanyika kwenye Ukumbi wa Majid, Kiembe Samaki visiwani Zanzibar jana, Maalim Seif ambaye ndiye Katibu Mkuu wa CUF alisema, Rais Kikwete amesababisha kuwepo kwa mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba.

Alisema, saa chache kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta uchaguzi huo, kituo kikuu cha kutangazia matokeo kilichokuweko Hoteli ya Bwawani kilizingirwa na vikosi vya jeshi na polisi na kwamba kitendo hicho kuwa ni “Mapinduzi ya Kikatiba”.

“Aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu wakati ule alikuwa Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete na ndiye aliyepeleka vikosi vile baada ya kuona chama chake kimeelekea kushindwa kwa upande wa Zanzibar,” alisema Maalim Seif na kuongeza;

“Dkt. Shein wala Balozi Seif (Seif Ali Idd) hawamiliki jeshi wala polisi, vile ni vikosi vya Dk. Kikwete wakati ule na hawezi kukwepa lawama ya kuingilia uchaguzi wa Zanzibar.”

Maalim Seif pia amewashutumu baadhi ya viongozi wakiwemo wa dini wanaojaribu kupotosha ukweli na kuunga mkono uamuzi batili wa kurejewa uchaguzi uliotangazwa na ZEC.

Akizungumzia kuhusu vikao vya kutafuta muafaka wa mkwamo wa kisiasa vilivyokuwa vikifanyika Ikulu ya Zanzibar, Maalim Seif alisema katika vikao hivyo walijadiliana na kukubaliana kuwa ZEC imepoteza sifa ya kusimamia uchaguzi.

Alisema, ameshangazwa na kitendo cha ZEC kutangaza uchaguzi wa marejeo, huku viongozi wa CCM walioshiriki mazungumzo hayo wakiunga mkono.
Akizungumzia hali ya kisiasa Zanzibar, Maalim Seif alisema, siasa za nguvu na kimabavu zinazoendeshwa na CCM hazitoisaidia Zanzibar na badala yake zinaweza kuzidisha mgogoro uliopo.

Kauli ya CUF kugomea uchaguzi uliotangazwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu, imeungwa mokono na viongozi hao wa wilaya na majimbo visiwani humo wakiwakilisha wananchi na wafuasi wa chama hicho.

Viongozi hao waliunga mkono hatua hiyo iliyotanguliwa na tamko lililotolewa na Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho tarehe 28 Januari mwaka huu.

Kwenye mkutano huo walieleza kuwa uchaguzi halali, huru na wa haki ulifanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana ambapo wananchi walio wengi walimchagua Maalim Seif na uchaguzi huo kufutwa bila sababu za msingi.

No comments: