Maalim Seif Azungumza na Viongozi wa CUF Kisiwani Pemba.....Asisitiza Kutoshiriki Uchaguzi wa Marudio - LEKULE

Breaking

5 Feb 2016

Maalim Seif Azungumza na Viongozi wa CUF Kisiwani Pemba.....Asisitiza Kutoshiriki Uchaguzi wa Marudio



Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka Wazanzibari na wapenda amani kuondoa shaka na kwamba, atatangazwa kuongoza visiwa hivyo.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo kwenye viwanja vya Nngoma Hazingwa, Chake Chake Pemba akiwa na viongozi wa wilaya, majimbo na jumuiya za chama hicho ikiwa ni siku moja baada ya kufanya mkutano wa namna hiyo Unguja.

Kiongozi huyo ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF amesema kuwa, ukweli umedhihiri ndani na nje ya nchi na kwamba hakuna sababu ya kutotangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana.

Amesema, “Jumuiya na waangalizi wote wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa wameshuhudia uchaguzi huo na kujiridhisha kuwa ulikuwa huru, haki na wa uwazi na wanaendelea kushikilia msimamo wao kutaka mshindi wa uchaguzi huo atangazwe.”

Amesisitiza kuwa CUF haitoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu kauli ambayo pia imeungwa mkono na wafuasi wa chama hicho Pemba kama ilivyokuwa Unguja.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amemtaja Maalim Seif kuwa kiongozi aliyebobea kisiasa na anayejali maslahi ya Wazanzibari.

Katika hatua nyingine mawakilishi na madiwani wateule wa CUF  wamepanga kwenda mahakamani kutetea nafasi zao.

Wameeleza kwamba, kwa kuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imewapa hati za ushindi baada ya kufanya uchaguzi mkuu tarehe 25 Oktoba 2015, mpaka sasa hakuna aliyejitokeza kupinga ushindi wao.

Hata hivyo, Maalim Seif amesema, viongozi hao waliochaguliwa na wananchi katika uchaguzi huo na kisha kupewa shahada zao, watakwenda mahakamani kutetea nafasi zao na kutoruhusu viongozi wengine wa ngazi hizo kuchaguliwa tena kwa vile wao wanavyo vielelezo vyote vya kuchaguliwa kwao.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi yaliyobandikwa katika vituo vya kupigia kura na kuthibitishwa na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo, majimbo yote 18 ya uchaguzi Kisiwani Pemba yalichukuliwa na CUF, sambamba na wadi zote 32 za uchaguzi.

No comments: