Jinsi Rubani Rodgers Gower Alivyouawa Na Majangili - LEKULE

Breaking

1 Feb 2016

Jinsi Rubani Rodgers Gower Alivyouawa Na Majangili


Siku moja baada ya kifo cha rubani Rodgers Gower (37) aliyekuwa anaendesha helikopta inayomilikiwa na Mwiba Holdings, baadhi vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti kuwa huenda bunduki iliyomuua ni ile iliyokuwa inatumika kuulia tembo.

Miongoni mwa vyombo hivyo ni magazeti ya Uingereza ya Daily Mail, The Guardian, The Sun, The Telegram, The Independent, Shirika la Habari la Ufaransa AFP na Shirika la Utangazaji la Marekani CNN.

Mbali na vyombo hivyo, jana asubuhi mwili huo ulifanyiwa uchunguzi ambao ulionyesha matundu manne ya risasi, moja kwenye mguu, mawili begani na jingine kwenye paji la uso ambako risasi iliingilia kichwani na haikuwa imetoka. 

Chanzo cha habari katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, ulikopelekwa mwili huo kilisema walipewa maagizo kuhakikisha hauondolewi hadi risasi iliyopo kichwani imeondolewa.

“Unajua huyu aliyefariki ni Mzungu, hata kama amefanyiwa postmoterm hapa anaweza kufanyiwa nyingine Aga Khan, Dar es Salaam na akifikishwa kwao Uingereza anafanyiwa tena, ndivyo walivyo wenzetu,” alisema.

Ijumaa iliyopita, Gower aliuawa kwa risasi wakati akiendesha helikopta hiyo kwenye doria dhidi ya majangili katika Pori la Akiba la Maswa, mkoani Simiyu akiwa pamoja na raia wa Afrika Kusini, Nicky Bester ambaye alinusurika kifo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema Serikali inaendelea na uchunguzi ili kuwabaini majangili waliohusika. 

Alivyouawa 
Daily Mail lilisema jana kuwa inawezekana hata bunduki iliyomuua Gower ni ile waliyokuwa wanatumia majangili hao kuua tembo. Lilieleza kuwa wakati Gower akiwa katika doria, aliona mabaki ya tembo wawili chini.

Gazeti hilo lilimnukuu Pra tik Patel, mmoja wa marafiki wa karibu marehemu, akisema wakati anaendelea na doria aliona tembo mwingine ambaye hakuwa ameuawa muda mrefu.

“Baada ya kuona hivyo, akataka ageuze ili wakamwangalie yule tembo, huku akijaribu kuona kama kuna majangili, ndipo mwanamume mmoja alitokea akiwa na bunduki na kupiga kwenye uvungu wa helikopta,” alisema Patel ambaye pia ni mfanyakazi mwenzake.

“Ile risasi ilitoboa uvungu wa helikopta na kupenya ndani, ikampiga rubani kwenye mguu na sehemu ya bega na uso kisha kutoboa paa la helikopta na kutoka nje … kutokana na uzito wa silaha iliyotumika kumuua, pengine ndiyo ileile ambayo majangili walitumia kuua tembo.”

Hata hivyo, gazeti la The Telegram, lilieleza kuwa bunduki iliyotumika kumuua Gower ni AK47.

“Alipokuwa anamkaribia tembo mmoja aliyeuawa, ndipo akapigwa risasi na kufariki kabla ya timu ya waokoaji kufika katika eneo hilo,” ilisema sehemu ya habari hiyo.

Mwanzilishi wa Mfuko wa Hifadhi wa Friedkin (FCF) aliyetoa taarifa kwa vyombo vya habari, Dan Friedkin ambaye aliwahi kufanya kazi na Gower alisema ni jambo la kusikitisha kuona rubani huyo, aliyekuwa katika operesheni ya kusaidia Tanzania kupambana na majangili ameuawa na haohao majangili.

The Guardian liliripoti kuwa jukumu kubwa la marehemu ambaye pia alikuwa mhasibu kitaaluma, lilikuwa kusafirisha watalii kwenye kambi mbalimbali za hifadhi.

Gower ambaye pia alihitimu masomo ya urubani wa helikopta mwaka 2004 London, Uingereza amekuwa akifanya doria kwa kushirikiana na wahifadhi kwa ajili ya kupambana na majangili kwenye hifadhi.

Akizungumzia mipango ya mazishi, Patel alisema jana kuwa suala hilo bado linajadiliwa na familia ya marehemu.

Hata hivyo, taarifa nyingine zilieleza kuwa mwili huo unatarajiwa kusafirishwa kwenda Uingereza kwa mazishi.


Chanzo cha kuaminika katika Mount Meru kilisema muda mfupi baada ya mwili huo kufikishwa, wakala wa kusafirisha miili ya raia wa kigeni alifika na kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Mwiba Holdings, iliyokuwa inamiliki helikopta hiyo. 

No comments: