Hakimu na Ofisa Elimu Wafikishwa Mahakamani Wakidaiwa Kula Rushwa - LEKULE

Breaking

11 Feb 2016

Hakimu na Ofisa Elimu Wafikishwa Mahakamani Wakidaiwa Kula Rushwa


Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kintinku wilayani Manyoni Mkoa wa Singida, Mahando Sabato amefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh350,000.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo, alifanya kitenda hicho ili amsaidie mlalamikaji kuifuta kesi iliyokuwa ikimkabili kijana wake.

Mkuu wa Takukuru, Wilaya ya Manyoni, Michael Sanga alidai kuwa Desemba 30, mwaka jana, ofisi yake ilipokea taarifa kutoka kwa mlalamikaji (jina limehifadhiwa), kuwa hakimu Sabato alikuwa akimuomba rushwa hiyo ili afute kesi ya wizi wa Sh400,000 iliyokuwa ikimkabili kijana wake.

Sanga alidai kuwa katika kufanikisha azma yake ya kula rushwa, hakimu huyo alifuta dhamana ya mtuhumiwa huyo na kuamuru apelekwe mahabusu ya Gereza la Wilaya ya Manyoni, kwa siku 21 wakati akiendelea na mambo mengine.

“Baada ya kubaini kwa hakimu Sabato amedhamiria kwa kiwango kikubwa kupokea rushwa hiyo, tuliweka mtego katika eneo la kituo cha mabasi cha Kintinku, ndipo tukamkamata akiwa na fedha za mtego huo wa hongo,” alidai Sanga.

Mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana hadi Februari 17, kesi yake itakafikishwa mahakamani kusomewa maelezo ya awali.

Wakati huohuo, Takukuru imemfikisha kortini Ofisa Elimu Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, Prochesius Mguli kujibu tuhuma ya kughushi nyaraka za malipo kwa walimu 22 wa shule za sekondari wilayani humo.

Akisoma mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo katika Mahakama ya Wilaya ya Kyela, Ofisa wa Takukuru , Thomas Msuta alidai kuwa kati ya Agosti 18 na 30 mwaka 2012, mshtakiwa alighushi majina ya walimu hao, alidai walihudhuria semina na kuwalipa Sh3.3 milioni.

Msuta alidai mshtakiwa huyo katika ripoti yake alighushi saini za walimu hao wakati hawakushiriki kwenye semina.

Mshtakiwa yupo mahabusu baada ya kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana.


Hakimu, Jacob Ndila aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 17 itakapotajwa tena. 

No comments: