Corruption Watch Yapinga Hukumu Ya Ufisadi Wa Benki ya Standard Dhidi Ya Serikali Ya Tanzania - LEKULE

Breaking

8 Feb 2016

Corruption Watch Yapinga Hukumu Ya Ufisadi Wa Benki ya Standard Dhidi Ya Serikali Ya Tanzania



Hukumu ya kesi ya rushwa ya mkopo uliotolewa na Benki ya Standard ya nchini Uingereza kwa Serikali ya Tanzania imepingwa na taasisi ya kimataifa inayopambana na ufisadi, Corruption Watch, ikisema kuwa benki hiyo ilijisalimisha kuepuka adhabu kali.

Hukumu hiyo inatokana na kashfa ya ufisadi ambayo benki hiyo ilihusika baada ya kushinda zabuni ya kuitafutia Tanzania mkopo wa dola 600 milioni za Marekani (sawa na Sh1.2 trilioni) kwa mauzo ya hatifungani kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini ikaliingiza tawi lake la hapa nchini, Stanbic katika kupata kamisheni, kinyume na taratibu.

Katika makubaliano hayo haramu, kampuni ya EGMA ililipwa dola 6 milioni (sawa na Sh1.2 bilioni) kwa maelezo kuwa ilitoa huduma za ushauri.

Taarifa ya awali iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Ufisadi (SFO) ya Uingereza, ilibainisha kuwa EGMA haikutoa ushauri wowote na kuhusishwa kwake ilikuwa ni njia ya kuwanufaisha viongozi wa Serikali waliokuwa na mamlaka na taratibu za kukamilisha muamala huo.

Kwa mujibu wa Corruption Watch, baada ya taarifa hiyo ya SFO, benki hiyo ilipaswa kushtakiwa mahakamani ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake, lakini Standard Bank ilitumia Sheria ya Ufisadi nchini humo kumtaka Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutofanya hivyo na kufanikiwa kumshawishi.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Uingereza, Jaji Mwandamizi wa Mahakama ya Southwark Crown, Brian Leveon aliidhinisha na kutumia Sheria ya Makubaliano ya Kutoshtakiwa (DPA) kuilipisha faini Benki ya Standard na hivyo kukwepa kushtakiwa na kukumbana na adhabu za mahakamani.

Hii ni mara ya kwanza kwa Uingereza kutumia sheria hiyo kwa moja ya kampuni zake kubwa, jambo lililosababisha wadau na wanaharakati wanaopinga ufisadi wa kitaasisi, kuikosoa hukumu hiyo kwa maelezo kuwa inaikandamiza Tanzania, ambayo ni nchi maskini inayoingizwa kwenye vitendo vya rushwa kwa mipango kutoka nje ya mipaka yake.

Taasisi ya Corruption Watch ya nchini humo imesema benki hiyo haistahili kupata unafuu unaotokana na sheria hiyo ya DPA kwa maelezo kwamba iliratibu rushwa hiyo na maofisa wake walihusika, hivyo haikustahili kupewa adhabu ndogo kwa kutumia sheria hiyo.

“Serikali ya Tanzania haitaridhika na uwajibikaji wa benki hii katika kukabiliana na uhalifu ilioutenda. Corruption Watch inaona kuwa Tanzania imepunjwa kiasi inachostahili kulipwa kutokana na ufisadi huu,” inasema taarifa ya Corruption Watch ya mwezi Desemba.

Katika kuthibitisha udogo wa fidia ambayo benki hiyo imekubali kuilipa Tanzania, taasisi hiyo imeeleza kuwa malipo halali yangeweza kuzidi mara kumi ya makadirio ya awali, endapo madhara yote ya udanganyifu uliofanywa yangezingatiwa.

Inasisitiza kuwa faini hiyo ilitakiwa ifike dola 80 milioni (zaidi ya Sh160 bilioni) pamoja na riba ya faida ya dola 10 milioni (zaidi ya Sh20 bilioni) kutokana na kilichochumwa na taasisi hiyo ya fedha.

Wakati hapa nyumbani Serikali ikiwa imetangaza kuwachukulia hatua za kisheria maofisa wake wote waliohusika kwenye sakata hilo, akiwamo aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ambaye pia likuwa mwenyekiti wa EMGA, Harry Kitilya, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya maofisa wa benki hiyo walioratibu upatikanaji wa hatifungani hiyo.

“Hakuna mtu yeyote aliyechukuliwa hatua za kisheria ama na benki yenyewe au mahakama kutokana na uzembe wa kushindwa kuzuia vitendo vya rushwa. Watu hawa wangali wanahudumu katika vyeo vya juu kwenye sekta ya huduma ya fedha hapa Uingereza. Wanapaswa kuchunguzwa kwa lengo la kuwapunguzia heshima yao ya kitaaluma,”inasema taarifa hiyo.

Kuhusu utekelezaji wa sheria uliotumika mpaka Benki ya Standard ikapewa DPA, taasisi hiyo imelalamikia utegemezi wa uchunguzi uliofanywa na benki husika juu ya kashfa hiyo. 

Imeeleza kuwa upo uwezekano mahakama na umma wakawa hawajaelezwa kinagaubaga uovu uliofanywa na kampuni hiyo.

Kwa vile uamuzi huu wa DPA ni wa kwanza kutolewa Uingereza na kutakiwa kutumika kama rejea kwa matukio yatakayofuata, taasisi hiyo imeonya kuhusu kifungu cha 7 cha Sheria ya Ufisadi kinachotoa adhabu kwa kampuni au mfanyakazi wake anayeshindwa kudhibiti vitendo vya rushwa dhidi ya wateja wake.

“Kitendo cha kushindwa kuwachukulia hatua maofisa waliohusika ni kosa kubwa kisheria na kitaaluma,” inasema ripoti hiyo ya Corruption Watch UK.

“DPA hii inadhihirisha kuwa kifungu cha 7 cha Sheria ya Ufisadi ndicho kinachotoa adhabu ndogo kwa wavunjaji wake, hivyo kutia wasiwasi kama kweli Uingereza imedhamiria kukomesha rushwa miongoni mwa kampuni zake.”

Inasema kuwa benki hiyo iliamua kutumia DPA kukwepa mkono wa mahakama ili kulinda maslahi yake ambayo ni pamoja na leseni ya biashara katika Jiji la Westminster, mpango wake wa kuuza hisa zake kwa benki ya China ya ICBC pamoja na kuendelea kuimiliki hatifungani ya Tanzania. 

==>Hivi ni baadhi ya Vipande vya Ripoti hiyo 

No comments: