Bomba Kubwa La Kusambazia Maji Kutoka Chanzo Cha Maji Cha Ruvu Chini Lafika Jijini Dar Es Salaam - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Tuesday, 16 February 2016

Bomba Kubwa La Kusambazia Maji Kutoka Chanzo Cha Maji Cha Ruvu Chini Lafika Jijini Dar Es Salaam


Juu na Chini - Mafundi wakiendelea na kazi ya kulaza mabomba ya Maji eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam. Mabomba hayo ambayo sasa yamekamilika kwa urefu wa kilometa 54.8 kati ya 55.9 yatatumika kusafirisha maji kutoka mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.


( Na. Aron Msigwa - Dar es salaam)
Huduma ya Usambazaji wa Maji Safi katika jiji la Dar es salaam inatarajiwa kuimarika kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu kufuatia kukamilika kwa kilometa 54.8 za mradi wa Ujenzi wa Bomba kubwa la kusambazia Maji kutoka chanzo cha Maji cha Ruvu Chini.

Mradi huo unajengwa na Kampuni ya JBG Gauff Ingenieure kwa gharama ya shilingi Bilioni 141 ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania una jumla ya urefu wa kilometa 55.9.

Akizungumzia mradi huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang’ingo amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa bomba hilo kuelekea matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi umefika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam na huku ikiwa imebakiza kilometa 1.1.

 Amesema ujenzi wa mradi huo kutoka mtambo wa Ruvu Chini ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani na kuongeza kuwa utakapokamilika utazalisha lita milioni 270 kwa siku kutoka lita milioni 182 ambazo zote zitasukumwa kuja jijini Dar es salaam.

 Aidha, amesema kasi ya mkandarasi ya kulaza bomba hilo inaridhisha licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazochelewesha kazi hiyo zikiwemo za ufinyu wa eneo linapojengwa bomba hilo kuwezesha mitambo kufanya kazi vizuri katika eneo la mbezi Beach, mvua zinazoendelea kunyesha ,changamoto ya makazi ya watu kuwa ndani ya mradi ambapo kulikuwa na kesi 17 Mahakamani zikihusisha madai mbalimbali ya wananchi katika maeneo hayo.

“Ni kweli zipo changamoto zilizosababisha mradi kukawia kumalizika zikiwemo za wananchi kufungua kesi 17  Mahakama ya Ardhi, hadi sasa DAWASA tumeshinda kesi 14  ndiyo maana tumepata haki ya kutumia njia hii kukamilisha upanuzi wa mradi” Amesema Mwang’ingo.

Ameongeza kuwa lengo la mradi huu nikuongeza uzalishaji wa maji na kuboresha huduma kwa wakazi wa maeneo ya uwekezaji (EPZ) Bagamoyo, Chasimba, Buma, Zinga, Kerege na Mpiji mkoa wa Pwani.

Maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni Bunju, Wazo, Salasala, Madale na Kinzudi Mbezi Juu, Goba, Kawe, Makongo, Mwenge, Msasani, Mikocheni, Mlalakua, Masaki, Sinza, Kijitonyama, Manzese, Konondoni, Magomeni, Kigogo na Vingunguti.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Kampuni inajenga bomba hilo nchini Muhandisi Eric Omuruli akizungumzia mradi huo amesema kuwa yeye kama Meneja mradi atahakikisha anashughulikia changamoto zilizopo ili kukamilisha kwa wakati.

Amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika eneo la mradi hasa eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam kampuni ya JBG Gauff Ingenieure inafanya kila linalowezekana ili mradi huo ukamilike mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.

“Tumejipanga kufanya kazi hadi usiku kupunguza muda,kazi iliyobaki ni ndogo, tunawahakikishia DAWASA tutaimaliza kazi hii mwishoni mwa mwezi huu” Amesisitiza.

Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang’ingo (katikati) akitoa ufafanuzi kuhusu maendeleo ya Mradi wa ujenzi  wa bomba hilo la kusafirishia Maji kutoka Ruvu Chini  kuelekea matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi ambao umefika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam 

Post a Comment