Bingwa wa Olimpiki katika kuogelea kuwafunda makocha, waogeleaji wa Dar Swim Club - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Monday, 15 February 2016

Bingwa wa Olimpiki katika kuogelea kuwafunda makocha, waogeleaji wa Dar Swim Club

Penny mara baada ya kushinda medali katika mashindano ya Olimpiki

Muogelaji nyota wa zamani wa dunia na mshindi wa medali ya dhahabu ya michezo ya Olimpiki kwa upande wa wanawake, Penelope “Penny” Heyns wa Afrika Kusini ataendesha mafunzo ya siku mbili ya kuogelea kwa makocha wa klabu maarufu ya mchezo huo hapa nchini, Dar Swim Club. 
Penny ambaye ni bingwa wa kihistoria wa michezo ya Olimpiki kwa staili ya ‘Breastroke’ atawasili nchini Alhamis akitokea  Afrika Kusini tayari kuendesha mafunzo hayo kwa makocha watano wa klabu hiyo. Katibu Mkuu wa Dar Swim Club, Inviolata Itatiro alisema jana kuwa maandalizi yamekamilika na klabu yao itagharimia mafunzo hayo kwa lengo la kuboresha viwango vya wachezaji wao na makocha kwa ujumla. 
Inviolata alisema kuwa makocha wao watakaoshiriki katika kozi hiyo kuwa ni Michael Livingstone, Ferick Kalengela, Radhia Gereza, Kanisi Mabena, Adam Kitururu, Simon Ngoya na Salum Mapunda. Alisema kuwa makocha wao wanasifa za ngazi ya juu ya ufundishaji wa mchezo huo, kutokana na kukua kwa kasi kwa mchezo huo, wameona bora wapate mbinu za kisasa ili kwenda na wakati. 
“Makocha wetu wote watano ni bora katika ufundishaji, waliwahi kupata mafunzo Dubai, Marekani na nchi mbalimbali, lakini klabu imeona kuendelea kuwapa mbinu zaidi ili kufikia malengo yetu ya miaka 10,” “Tunataka kuona kila mtoto anacheza mchezo wa kuogelea, tulianza na watoto wadogo ambao kwa sasa ni mastaa katika mchezo huo na kuweza kushinda medali mbalimbali nje ya nchi,” alisema Inviolata. 

Alisema kuwa wao wameamua kupromoti mchezo wa kuogelea kwa vitendo ili kuona siku moja watanzania wanafuzu kushindana michezo ya Olimpiki, Jumuiya ya madola na mashindano ya dunia siyo kupata nafasi za upendeleo kama ilivyo sasa. Alifafanua kuwa Penny alitwaa medali za dhahabu katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika mjini Atlanta 1996 kwa mita 100 na 200 na wanaamini kuwa ujio wake utapandisha morali wachezaji wao na makocha.
Post a Comment