Ban Ki Moon: Nkurunziza amekubali kufanya mazungumzo na upinzani - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Wednesday, 24 February 2016

Ban Ki Moon: Nkurunziza amekubali kufanya mazungumzo na upinzani


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amekubali kufanya mazungumzo na upande wa upinzani kuumaliza mzozo wa kisiasa nchini humo.
Ban ambaye anafanya ziara yake ya kwanza Burundi tangu mzozo kuzuka nchini humo mnamo mwezi Aprili mwaka jana, aliwasili jana alasiri na leo amefanya mazungumzo na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza mjini Bujumbura.
Mkutano huo unakuja baada ya Katibu huyo wa Umoja wa Mataifa kukutana na viongozi wa vyama vya kisiasa na wa asasi za kiraia katika juhudi za kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Burundi ambao umedumu kwa miezi kumi.
Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa amesema ziara ya Ban ni muhumu sana kwani wanatumai atamshinikiza Rais Nkurunziza hatimaye kukubali kufanya mazungumzo ya kina na yasiyo na masharti na wapinzani wake.
Ban Kuzuru Congo na Sudan Kusini(P.T)
Baada ya mazungumzo hayo na Rais Nkurunziza, Ban ataizuru Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na pia Sudan Kusini ambako kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwezi Desemba mwaka 2013.
Ban anatarajiwa kuzifufua juhudi zinazodhamiria kupatikana kwa suluhisho la amani kwa mzozo wa kisiasa wa Burundi ambao ulichochewa na azma ya Nkurunziza kugombea muhula wa ttau madarakani kinyume na sheria.
Serikali ya Burundi inaonekana kulegeza msimamo wake dhidi ya wapinzani wake kwa kukubali ujumbe wa viongozi wa nchi za Afrika wanaotarajiwa kuwasili nchini humo baadaye wiki hii na kufutilia mbali waranti za kimataifa za kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani.
Saa chache kabla ya kuwasili kwa Katibu huyo wa Umoja wa Mataifa, watu wawili waliuawa na wengine tisa walijeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na washambuliaji waliokuwa katika pikipiki.
Meya wa mji wa Bujumbura Freddy Mbonimpa ambaye ameyalaani mashambulizi hayo na kuyataja vitendo vya kigaidi vinavyowalenga raia wasio na hatia amesema mji huo umekuwa mtulivu kwa siku kadhaa zilizopita.
Mbonimpa amesema washambualijai hao wamefanya mashambulizi hayo ili kudhihirisha uwepo wao wakati ambapo Burundi inamtarajia mgeni muhimu.
Haijabainika wazi ni nani hasa aliyehusika katika mashambulizi hayo ya maguruneti ambayo yameongezeka katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita. Maafisa wa usalama, waasi na upinzano wanalaumiana kwa mashambulizi hayo yanayosababisha mauaji.
Wakati huo huo, Ufaransa imewasilisha pendekezo katika Umoja wa Mataifa la kupelekwa kwa askari wa Umoja huo nchini Burundi ili kutuliza ghasia.
Marais wa Afrika kuzuru Burundi
Ufaransa inatumai kuwa pendekezo hilo litaidhinishwa kabla ya marais wa Afrika wakiongozwa na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kuwasili Burundi siku ya Alhamisi wiki hii kwa mazungumzo na Nkurunziza.
Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Francois Delattre amesema wanataka kuchukua fursa ya kuwepo juhudi za pamoja za jumuiya ya kimataifa kukomesha ghasia na kutafuta suluhisho la tija Burundi.
Mzozo huo wa Burundi umesababisha vifo vya zaidi ya watu 400 na wengine zaiidi ya 240,000 wamelazimika kutorokea nchi nyingine. Maelfu ya watu wamekamatwa na maafisa wa usalama wanashutumiwa kwa kuwaua watu kiholela na kukiuka haki nyingine za kibinadamu.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa Burundi iko katika hatari ya kutumbukia tena katika vita vya wenyewe kama vilivyoshuhudiwa kati ya mwaka 1993 hadi mwaka 2005 ambapo kiasi ya watu laki tatu waliuawa.
Chanzo:DW
Post a Comment