Wizara ya Afya yatoa Taarifa ya Ugonjwa wa Kipindupindu Nchini. - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Monday, 11 January 2016

Wizara ya Afya yatoa Taarifa ya Ugonjwa wa Kipindupindu Nchini.

 Na Skolastika Tweneshe-Maelezo
Jiji la Dar es salaam limeripotiwa kutokuwa na mgonjwa yoyote wa kipindupindu  kuanzia Desemba mwaka jana.

Akizungumza leo na waandishi wa habari  jijini Dar es salaam  Naibu waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto Mh. Dkt Hamisi  Kigwangalla amesema kuwa licha ya ugonjwa wa kipindupindu kuanzia jijini Dar es salaam na kudumu kwa miezi minne lakini kwa sasa hajaripotiwa mgonjwa wa kipindupindu.

“Mkoa wa Dar es salaam ambako ndipo ugonjwa ulipoanzia na kudumu kwa miezi minne haujaripotiwa  kuwa mgonjwa wa kipindupindu kuanzia tarehe 22/12/2015,” alisema Kigwangalla.

Waziri Kigwangalla aliongeza kuwa mikoa mingine ambayo haijaripotiwa kuwa na maambukizi kwa muda wa wiki moja ni pamoja na Mbeya,Rukwa,Katavi,Kigoma,Kagera  na Lindi.

Aidha  alisema kuwa mikoa ambayo haijarioptiwa ugonjwa huo kwa zaidi ya miezi miwili iliyopita ni  Shinyanga, Kilimanjaro na Iringa  pia amesema kuwa kuna mikoa ambayo haijawahi kuripoti tangu ugonjwa wa kipindupindu uanze nayo ni mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mtwara.

Dkt. Kigwangalla alitaja mikoa iliyotoa idadi kubwa ya wagonjwa wa kipindupindu ambayo ni Halmashauri ya Morogoro(66), Arusha (50), Singida(40), na manispaa ya Dodoma (33).

Pia amewaasa wananchi  kunywa maji yaliyo safi na salama, kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama pamoja na kunawa mikono na maji safi na sabuni kwa maji safi yanayotiririka pamoja na kutumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji ,maziwa na mabwawa.


Kwa mujibu wa wizara ya afya tangu ugonjwa wa kipindupindu uanze, jumla ya watu 13,491 wameugua kipindupindu, na kati yao watu 205 wameshafariki kutokana na  ugonjwa huo.
Post a Comment