Waziri Simbachawene Amsimamisha Kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma - LEKULE

Breaking

26 Jan 2016

Waziri Simbachawene Amsimamisha Kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mh. George Simbachawene amemvua madaraka Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma, Bw. Augustino Kalinga kufuatia kuruhusu ofisi yake kuwachangisha wazazi michango ambayo serikali imezuia katika kutoa elimu ya msingi bila malipo.

Mh. Simbachawene alifikia uamuzi huo jana mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali baada ya kugundua kuwa manispaa ya Dodoma imesambaza barua kwa walimu wakuu wa shule za msingi ambazo zimeagiza kuwatoza wazazi michango ya maji, umeme na mlinzi ambayo imekatazwa na serikali.

Amesema kuwa Bw. Kalinga amevuliwa madaraka yake baada ya kubainika kuwa ameshindwa kuwasimamia watumishi walio chini yake hadi kusababisha kuandika barua na kusambaza kwa walimu wakuu wa shule za msingi katika manispaa ya Dodoma ambayo inatofautiana na maelezo ya serikali yaliyopo kwenye mwongozo.

Aidha, amebainisha kuwa katika mwongozo wa elimu ya msingi uliotolewa na serikali unafafanua majukumu ya wazazi na walezi ambayo wanatakiwa kuyafanya kuwa ni pamoja na sare za shule, vifaa vya michezo na vya kujifunzia pamoja na matibabu na chakula.

No comments: