Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye Aruhusiwa Kutoka Hospitali - LEKULE

Breaking

16 Jan 2016

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye Aruhusiwa Kutoka Hospitali


WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyekuwa amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyoko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ameruhusiwa kurudi nyumbani.

Ofisa Uhusiano Msaidizi wa MNH, John Steven, jana alisema Sumaye aliruhusiwa juzi jioni baada ya madaktari kuridhishwa na maendeleo ya afya yake.

“Sumaye amepewa ruhusa ya kurudi nyumbani tangu juzi jioni, madaktari wake waliridhishwa na mwenendo wa afya yake kutokana na matibabu waliyompatia dhidi ya ugonjwa uliokuwa unamsumbua,” alisema.

Hata hivyo, Steven hakufafanua ugonjwa uliokuwa ukimsumbua kiongozi huyo mstaafu kwa kile alichoeleza kuwa kanuni na sheria za kitabibu zinakataza.

“Siwezi kutaja ugonjwa uliomfanya akalazwa hapa, mwenyewe anaweza kuwaeleza kwa sababu ni siri yake na daktari wake,” alisema.

Sumaye alilazwa hospitalini hapo Januari 7, mwaka huu na Januari 11, Rais John Magufuli, alimtembelea hospitalini hapo na kumpa pole.


Mapema mwaka huu, Sumaye alitangaza rasmi kujiunga na Chadema baada ya kuondoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka jana muda mfupi kabla ya kampeni za uchaguzi.

No comments: