Waziri Mkuu Majaliwa Kutikisa Mkoa wa Ruvuma Kwa Siku 3 Kuanzia Leo - LEKULE

Breaking

3 Jan 2016

Waziri Mkuu Majaliwa Kutikisa Mkoa wa Ruvuma Kwa Siku 3 Kuanzia Leo


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo ataanza ziara ya siku tatu mkoani Ruvuma, kuhimiza na kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo. Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa, Said Mwambungu alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Songea jana.

Alisema, Waziri Mkuu atawasili katika Uwanja wa Ndege wa Songea saa 6 mchana, ambapo atapokelewa na viongozi wa serikali na vyama vya siasa. Mwambungu alisema atakapowasili mjini Songea, Waziri Mkuu atakwenda moja kwa moja Ikulu Ndogo kisha kusomewa taarifa ya mkoa.

Kesho asubuhi Waziri Mkuu atafungua Benki ya Posta Tawi la Songea na kutembelea Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma mjini Songea, ambapo atakagua kila kitengo na kuzungumza na wafanyakazi wa hospitali. Pia Waziri Mkuu atazungumza na watumishi wa idara zote za serikali waliopo mjini Songea.

Mwambungu alisema baada ya kumaliza kuzungumza na watumishi hao, atatembelea Kitengo cha Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) na kukagua maghala yanayotumika kwa ajili ya kuhifadhi chakula.

Aidha, atatembelea kuona ujenzi wa makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Songea Vijijini katika kijiji cha Lundusi kata ya Maposeni na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara. Mkuu huyo wa mkoa alisema keshokutwa Waziri Mkuu atafanya majumuisho ya ziara yake mjini Songea.

Mwambungu aliomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote ambayo Waziri Mkuu atatembelea, ikiwemo barabarani, ili kumlaki. Hii itakuwa ni ziara ya pili ya kiserikali ya Waziri Mkuu, tangu alipoteuliwa kushika wadhifa.

Wiki iliyopita alikuwa mkoani Kigoma, alikotembelea miradi mbalimbali na kukutana na wafanyakazi wa idara mbalimbali za serikali, kufanya mikutano ya hadhara na kuzungumza na wananchi.

Akiwa huko, Waziri Mkuu Majaliwa alibaini kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha za umma, unaohusisha uuzwaji wa jengo la Shirika la Maendeleo Kigoma (KIGODECO) kwa bei ya kutupwa.

Majaliwa alitoa siku mbili kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Dk John Ndunguru kukamilisha uchunguzi wake na kumpatia taarifa ya maandishi juu ya tuhuma za ubadhirifu huo.


Aliagiza pia uchunguzi juu ya uuzaji wa viwanja 12 vya Manispaa ya Kigoma/Ujiji, unaodaiwa kukiuka taratibu. Alitoa maagizo hayo Desemba 30, mwaka jana wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa huo, alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku mbili.

No comments: