Waziri Mkuu Awaonya Wanyonyaji wa Wakulima....Aziagiza Halmashauri Kujenga Vituo vya Ununuzi Vijijini Badala ya Kuendelea Kutumia Mawakala - LEKULE

Breaking

5 Jan 2016

Waziri Mkuu Awaonya Wanyonyaji wa Wakulima....Aziagiza Halmashauri Kujenga Vituo vya Ununuzi Vijijini Badala ya Kuendelea Kutumia Mawakala


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea, wakati akiendelea na ziara yake mkoani Ruvuma. 
 
Akizungumza na wafanyakazi wa Wakala hiyo, wadau wa kilimo pamoja na wananchi jana, (Jumatatu, Januari 4, 2016) nje ya majengo ya Wakala mara baada ya kukagua mahindi yaliyohifadhiwa katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea , mkoani Ruvuma alisema kufuatia taarifa ya kuwepo na baadhi ya maeneo yenye njaa nchini, Serikali imetoa tamko kuwa hakuna mtanzania atayakekufa kwa njaa. 
 
Alisema serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa imeweka mikakati ya kukabiliana na tatizo la njaa kwa kutoa msaada wa chakula katika maeneo yanayokabiliwa na njaa. 
 
“Ni wajibu wangu kuhakikisha nasimamia vizuri hili, nimeona hali ya uhifadhi wa chakula, tunayo mahindi ya kutosha lakini hakuna sehemu ya kuhifadhi chakula” alisema Waziri Mkuu.
 
Waziri Mkuu Majaliwa aliendelea kwa kusema uwezo wa maghala hayo yaliyopo chini ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea yana uwezo wa kuhifadhi tani 29 pekee na Songea inauwezo wa kuzalisha zaidi tani 70 hadi 80. 
 
Pia , aliagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea , kuanzia mwaka huu kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa pamoja na Wakuu wa Wilaya kuanzisha vituo vya kununulia mahindi vijijini na kuhakikisha magunia yanawafikia wakulima katika vituo hivyo ili kuwapunguzia mzigo wakulima wa kusafirisha mahindi yao na kuwafanya wayauze kwa bei ya  soko.
Alisema wakulima  wamekuwa wakitumia gharama kubwa kuyasafirisha mahindi katika maeneo ya kuyauzia ambapo wengine wamekuwa wakishindwa na kuwanufaisha mawakala ambao wamekuwa wakiyauza kwa niaba yao. 
 
 Waziri Mkuu pia, ameitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea ,kutumia teknolojia ya kisasa ya uhifadhi wa chakula, kuandaa utaratibu maalum utakaozuia msongamano wa malori yanayosubiri kupata huduma ya kununua mahindi nje ya majengo ya Wakala na kukamilisha miradi itakayosaidia Wakala kuwa na fedha za kutekeleza majukumu yake. 
 
Kwa upande wake, Meneja Hifadhi wa Chakula kanda ya Songea, Bwana. Morgan Mwaipaya alisema kati ya maghala 33 ya kuhifadhi mahindi nchi nzima, Songea ina maghala 6 kati ya hayo. 
Alisema Wakala imeweka vipaumbele vyake ambavyo ni pamoja na kutoa chakula cha msaada kwa maeneo yenye matatizo ya njaa, kuongeza upatikanaji wa mahindi ili kuzuia kupanda kwa bei ya chakula mwaka 2015 – 2016, Wakala kununua na kuhifadhi mahindi katika maeneo yaliyozalisha zaidi na kuzingatia sehemu ya sehemu ya akiba ya chakula na kuuza kwa wakulima, mawakala pamoja na Wakala wa Chakula duniani (World food program).
Alisema Wakala imeandaa mikakati ya mbalimbali ikiwemo kuongeza uwezo wa tani 24600 hadi tani 45000 kwa mwaka 2014- 2017, kuboresha mfumo wa utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya stahili ya TEHAMA na kutumia fursa za mikopo kutoka Taasisi mbalimbali za kifedha ili kuendesha shughuli za uwezeshaji ikiwemo kuelimisha taratibu za ununuzi kwa mawakala. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mahindi yaliyohifadhiwa nje ya majengo ya maghala ya  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA mjini Songea  akiwa katika ziara ya siku tatu mkoani Ruvuma Januari 4, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mahindi yaliyohifadhiwa nje ya majengo ya maghala ya  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA mjini Songea  akiwa katika ziara ya siku tatu mkoani Ruvuma Januari 4, 2016. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Jego la Halmashauri ya Wilaya ya Peramiho akiwa katika ziara ya mkoa wa Ruvuma Januari 4, 2015.  

No comments: