Uturuki: shambulio la kujitoa mhanga Istanbul - LEKULE

Breaking

13 Jan 2016

Uturuki: shambulio la kujitoa mhanga Istanbul


Polisi inatoa ulinzi katika eneo kulikotokea mlipuko karibu na eneo takatifu la St Sophia na Msikiti wa Blu, Januari 12, 2016.

Na RFI
Mlipuko mkubwa umetokea Jumanne hii Januari 12, 2016 katika kituo cha utalii cha Sultanahmet katika mji wa Istanbul, karibu na Msikiti wa Blu na makavazi ya St Sophia.
Watu wasiopungua 10, wengi wao wakiwa Wajerumani wameuawa, na wengine 15 wamejeruhiwa. Waziri mkuu amesema kuwa mshambuliaji, ni raia wa Syria, ambaye alizaliwa mwaka 1988, na ni mwanamgambo wa kundi la Islamic State.
Shambulio lililotokea Jumanne hii asubuhi limeligusa eneo lenye ishara kubwa katikati mwa mji wa Istanbul, eneo ambalo ni la kitalii la Sultanahmet. Kwa mujibu wa mwandishi wetu katika mji wa Istanbul, Alexander Billet, mlipuko huo ulikua mkubwa kwani ulisikika hata katika miji mbalimbali jirani barani Asia.
Waathirika wengi ni Wajerumani
Vyombo vya habari vya Uturuki awali vilibaini kuwa watu kadhaa walijeruhiwa, wala hakuna aliyepoteza maisha, lakini mlipuko huo umesababisha vifo vya watu wasiopungua 10. Wengi wa watu waliopoteza maisha ni wageni. Mapema mchana, Waziri mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, amewasiliana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ili kumuarifu kuwa wengi mwa waliopoteza maisha ni raia wa Ujerumani. Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imewashauri raia wake kuepuka maeneo ya kitalii ya Istanbul. Ubalozi wa Norway umesema kuwa mmoja wa raia wake ni pia miongoni mwa watu waliopoteza maisha.
Waziri mkuu Ahmet Davutoglu ameendesha mkutano kuhusu hali hiyo Jumanne hii asubuhi na waziri wa mambo ya ndani pamoja na mkuu wa Idara ya Ujasusi. Kwa mujibu wa Naibu Waziri mkuu wa Uturuki Numan Kurtulmus, mamlaka ya nchi hiyo imemtambuliwa muhusika wa shambulio hilo, mshambuliaji wa kujitoa mhanga anayeelezwa kuwa ni raia wa Syria, ambaye alizaliwa mwaka 1988. Katika hotuba fupi kwenye runinga ya taifa, Ahmet Davutoglu amesema kuwa ni mwanamgambo wa kundi la Islamic State. Mapema mchana, wakati wa hotuba yake kwa taifa, rais wa Uturuki mwenyewe amelaani "shambulio hilo la kujitoa mhanga".

No comments: