Simbachawene Aapa Kuweka Historia Mpya .....Asema Ndani Ya Miaka Miwili Hakuna Mwanafunzi Atakaye Kaa Chini Kwa Kukosa Dawati - LEKULE

Breaking

23 Jan 2016

Simbachawene Aapa Kuweka Historia Mpya .....Asema Ndani Ya Miaka Miwili Hakuna Mwanafunzi Atakaye Kaa Chini Kwa Kukosa Dawati



Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene amesema atahakikisha shule zote hapa nchini zinakuwa na madawati yanayofanana.

Alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia changamoto za elimu bila malipo iliyoanza kutolewa Januari mwaka huu.

“Katika historia ninayotaka kuandika ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini katika kipindi cha miaka miwili lazima tuondokane na tatizo hili,” alisema na kuongeza kuwa atakuja na ubunifu utakaoondoka tatizo hilo nchini.

“Nataka kuwe na madawati yanayofanana nchi nzima yenye lebo ya For Government Primary School, ninaona mwanga mkubwa mbele yangu na katika hili ninaweza kufanikiwa nipeni fursa,” alisema.

Alisema pia kumekuwa na changamoto kubwa ya matumizi ya fedha zilizopelekwa kwa ajili ya kugharamia elimu na kuongeza lengo la serikali kutoa elimu bila malipo litabaki pale pale kwani miaka ya nyuma watoto wengi walishindwa kupata elimu kutokana na gharama kuwa kikwazo kwao.

Simbachawene alisema changamoto kubwa ni kwa walimu kudhani fedha zilizopelekwa shuleni ni za mwaka mzima lakini ukweli ni kuwa fedha ni za kila mwezi.

Alisema kila mwanafunzi wa shule ya msingi ya serikali atatoa shilingi 10,000 na kwa sekondari ni shilingi 25,000 kwa mwaka kwa ajili ya uendeshaji wa shule.

Waziri huyo alisema kwa shule za sekondari za kutwa kila mwanafunzi atapata shilingi 3,540 na kwa shule ya sekondari ya bweni ni shilingi 7,243.

“Ukiwa na wanafunzi 500 maana yake shule inapata zaidi ya shilingi milioni 3.6 kwa mwezi mmoja tu je ukipata fedha hizo unashindwa kuendesha shule?” alisema na kuongeza kuwa serikali pia ilipeleka fedha za chakula ili watoto waweze kula lakini fedha hizo zisitumike kulipa madeni ya samani ya wazabuni.

Aliwataka walimu wasivunje moyo juhudi zinazofanywa na serikali kwani mzazi masikini amepokea mzigo mzito sana na serikali.

“Tutakapokuja kwenye bajeti ya kwanza ya awamu ya tano tutakuwa tumejifunza changamoto. Tutaboresha na mambo mengine mazuri yatakuja,” alisema.

No comments: