Serikali Yatangaza Mkakati wa Kuwafilisi Mafisadi na Wahujumu Uchumi - LEKULE

Breaking

28 Jan 2016

Serikali Yatangaza Mkakati wa Kuwafilisi Mafisadi na Wahujumu Uchumi



SERIKALI kupitia vyombo vyake vya dola, imetangaza kuzitaifisha mali za wote waliopatikana na hatia ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi na kueleza kuwa utaratibu huo ndio utakaoendelea kwa watuhumiwa ambao bado kesi zao hazijamalizika au hazijapelekwa mahakamani.
  
Tangazo hilo la serikali limetolewa leo Januari 28, 2016 na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, DPP, Bw. Biswalo Mganga, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi(DCI), Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani na Mkurugenzi wa Upeleelzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakati wa mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam.
 
Katika kuhakikisha kuwa jukumu hilo linatekelezwa, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai amesema, mwaka 2012 idara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa pamoja walikubaliana kufanya kazi ya ufuatiliaji wa mali zinazohusiana na uhalifu kama sheria inavyotaka na kwa upande wa jeshi hilo tayari kitengo chake cha upelelezi wa makosa ya uhalifu wa kifedha (Money laundering) kiko kazini.
 
“Katika kutekeleza mkakatihuo, Jeshi la Polisi limekamilisha upelelezi wa kesi 23 ambazo ziliwasilishwa kwa DPP na kati ha hizo ,kesi tatu (3) zimetolewa uamuzi na nyingine ishirini ziko katika hatua ya maombi ya kupata amri ya Mahakama ili ziweze kuzuiwa au kutaifishwa (Restraint or confiscation).” Alifafanua Kamishna Diwani Athumani
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi kutoka TAKUKURU, Bw. Alex Mfungo, yeye amesema, taasisi yake imeona hakuna maana yoyote kwa mhalifu wa Ufisadi na uhujumu uchumi ukamfunga gerezani na kisha kumuachia baada ya kifungo halafu aendelee kutumia mali alizochuma kwa njia za haramu.

“Tumeona njia mbadala ya kudhibiti hali hiyo na kwa mujibu wa sheria ni kumfilisi mhusika hata kama atatumikia kifungo.” Alibainisha Bw. Alex

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka, DPP, Bw. Biswalo Mganga, yeye amesema ili kuendana na dhana ya Hapa Kazi Tu, ni lazima kukabiliana na wahujumu uchumi na Mafisadi ili hatimaye Wananchi walio wengi waweze kunufaika na rasilimali zao. 

“Natoa wito kwa nyie waandishi wa habari muujulishe umma wa Watanzania kuwa kama mtu anayo taarifa au anajua mali zinazomilikiwa na mtu isivyo halali hususan watumishi wa umma basi atoe taarifa.”Alisema
 Mkurugezni wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga
DCI Kamishna wa Polisi Diwani Athumani
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU, Bw. Alex Mfungo
DCI Kamishna wa Polisi Diwani Athumani
Bw. Mfungo, (kulia), akiwa na DPP, Mganga (Picha na K-VIS MEDIA/Khalfan Said)

No comments: