Serikali Kutoa Bei Ekezi Uuzaji Ardhi Ili Kuwawezesha Wananchi Wasio Na Uwezo Kiuchumi - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Tuesday, 12 January 2016

Serikali Kutoa Bei Ekezi Uuzaji Ardhi Ili Kuwawezesha Wananchi Wasio Na Uwezo Kiuchumi


SERIKALI inatarajia kutoa bei elekezi ya uuzaji wa ardhi, tofauti na hali ya sasa ambayo viwanja vimekuwa vikiuzwa kwa bei ya juu na kufanya watu wasio na uwezo kiuchumi kushindwa kumiliki na kujenga nyumba.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Wiliam Lukuvi alisema jana kwamba serikali inaandaa utaratibu wa kutoa bei hiyo elekezi, itakayohusu watu wote.

Alitoa taarifa hiyo jana mjini Kibaha katika mkoa wa Pwani, wakati alipofanya ziara ya siku moja ya kutaka kufahamu kero mbalimbali zilizo kwenye Idara ya Ardhi katika mkoa wa Pwani, zinazokabili wananchi.

Alisema bei dira hiyo itakuwa kwa watu wote wanaouza ardhi kwa maana kwamba, kabla ya kuuza, watatakiwa kuwasiliana na serikali ili wananchi wapunguziwe kero ya kushindwa kumiliki ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo. Alisema ardhi ni huduma na si biashara.

Waziri Lukuvi alisema baadhi ya watu wamefanya ardhi, kama ndiyo sehemu ya kujinufaisha kwa kununua mashamba, kisha kuyagawa viwanja ambavyo huviuza kwa bei kubwa. Alisema jambo hilo limekuwa likisababisha wananchi wa kawaida, kushindwa kumudu kununua viwanja.

“Msifanye ardhi kama biashara. Hii ni huduma na huduma haipaswi kutozwa gharama kubwa. Utashangaa eneo kama Kibaha, kiwanja kinauzwa kiasi cha shilingi milioni kumi. Kwa mtu wa hapa ana uwezo gani?” alisema.

Aliendelea kusema, “Kwa mfano, pale Kibada viwanja vilikuwa vikiuzwa kwa shilingi milioni tatu tu hatuwezi kukubali hali hii iendelee.”

Alisema hata wale ambao wamewekeza ardhi kwa muda mrefu na kufanya kama rehani kwa ajili ya kukopa fedha kwenye benki zao, wamekuwa ni tatizo kubwa.


Alieleza kwamba, wengi wao wanaoomba mashamba makubwa serikalini, wamekuwa wakibadili mashamba hayo na kuwa viwanja ambavyo huviuza kwa bei mbaya. “Na ni hao hao wanamiliki maeneo mbalimbali hapa nchini kwani majina ni yale yale,” alisema.
Post a Comment