Sakata la Upotevu wa Makontena Bandari Lachukua Sura Mpya Baada ya Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa) Kufungua Kesi Mahakama Kuu - LEKULE

Breaking

3 Jan 2016

Sakata la Upotevu wa Makontena Bandari Lachukua Sura Mpya Baada ya Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa) Kufungua Kesi Mahakama Kuu


Sakata la utoaji makontena bila kulipia tozo ya bandari, limechukua sura mpya baada ya Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa) kufungua kesi Mahakama Kuu, kupinga kitendo cha Mamlaka ya Bandari (TPA) kuwadai fedha za tozo hiyo ambazo wamesema wameshalipia.
 
Taffa imefungua kesi hiyo kwa hati ya dharura, ikipinga TPA kutaka kufungia kampuni zinazojihusisha na masuala ya forodha, kuwakamata watendaji wake, na kutaka iache kushinikiza walipe tena tozo hizo.
 
TPA imezitaka taasisi 284 kuwasilisha nyaraka za malipo ya tozo hizo za kuanzia mwaka 2014, kuthibitisha kama zilikuwa zikilipa.
 
Tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa afanye ziara mbili za kushtukiza bandarini na baadaye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, zimeibuliwa kashfa nyingi za ufisadi, na hasa upitishaji wa makontena bila ya kulipia kodi na mengine kutoweka.
 
Akizungumza katika mkutano mkuu wa dharura wa chama hicho uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, wakili anayesimamia kesi hiyo, Lambaji Madai aliwataka wanachama wa Taffa kuendelea kuwasilisha ushahidi wa malipo ya tozo hizo wanayofanya kupitia benki, ili yaweze kutumika kama kidhibiti mahakamani.
 
“Tunapaswa kuwa kitu kimoja katika hili na tuache kurushiana maneno wenyewe kwa wenyewe. Si wakati wa kuangalia nani msafi na nani mchafu kati yetu. Mawakala wa forodha ndiyo tunatuhumiwa na sehemu pekee ya kusikilizwa sisi na TPA ni mahakamani,” alisema.
 
Alisema kuanzia Jumatatu ijayo watapata mrejesho wa kesi hiyo, na kwamba lengo ni kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa kuwa mawakala wa forosha wanaonekana kuhusishwa na mambo ambayo hawayafanyi.
 
Rais wa Taffa, Stephen Ngatunga alisema TPA imekuwa ikiwatuhumu mawakala wa forodha wanaolipa tozo hiyo kwa niaba ya wateja wao, kuwa ndiyo wahusika, wakati inajulikana wazi kuwa mzigo hauwezi kutoka bandarini bila kuonyesha stakabadhi za malipo yaliyofanywa kwenye benki zenye mikataba na mamlaka hiyo.
 
“Jumatatu (kesho) tutakwenda Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwasilisha malalamiko yetu na kueleza jinsi TPA na benki wanavyoshirikiana kufanya wizi huu. Tuna ushahidi na hawa watu wanaiba hata ukifanya malipo kwa fedha taslimu au hundi,” alisema Ngatunga, huku baadhi ya mawakala wakionyesha ushahidi wa malipo.
 
Alisema ili kutatua tatizo hilo, wadau wote wa usafirishaji wanapaswa kukutana na kujadili ili kuwabaini wahusika, si kuwatupia mpira mawakala wa forodha.
 
“Jiulizeni iweje TPA wazitake kampuni za forodha ziwapelekee ushahidi wa malipo wakati wao ndio wanaotoza malipo hayo na wana kumbukumbu,” alisema Ngatunga.
 

Baadhi ya mawakala waliozungumza katika mkutano huo walipendekeza masuala mbalimbali, ikiwamo kutaka kufanya malipo hayo kwenye Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Mamlaka ya Mapato (TRA), badala ya kutumia benki.

No comments: