Profesa Muhongo Awataka EWURA NA TANESCO Waongeze Kasi Kazini.....Aagiza Waharakishe Kushughulikia Maombi ya Wawekezaji - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Friday, 8 January 2016

Profesa Muhongo Awataka EWURA NA TANESCO Waongeze Kasi Kazini.....Aagiza Waharakishe Kushughulikia Maombi ya Wawekezaji


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kutafuta uwezekano wa kufupisha muda wa kushughulikia maombi ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika uzalishaji umeme.

Alitoa agizo hilo hivi karibuni jijini Dar es Salaam alipokutana na Viongozi wa mashirika hayo kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uwekezaji katika sekta ya nishati.

Profesa Muhongo alisema utaratibu unaotumika sasa katika kushughulikia maombi ya wawekezaji katika sekta ya nishati unachukua muda mrefu hali inayosababisha usumbufu kwa wawekezaji.

“Utaratibu wa kutumia muda mrefu kiasi cha miezi sita au zaidi kushughulikia maombi ya wawekezaji haufai. Sisemi mvunje sheria kwa kutofuata utaratibu au kutumia njia za mkato, lakini inabidi mtafute namna ya kushughulikia maombi husika kwa haraka,” alifafanua Waziri Muhongo.

Ili kuhakikisha sheria inazingatiwa wakati wa kutekeleza agizo hilo, Waziri aliwataka Watendaji hao pamoja na mambo mengine kufuatilia ili kujua Sheria ya Manunuzi Serikalini inatoa mwongozo upi katika suala husika.

Waziri Muhongo alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha nchi inafikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 na hivyo ni lazima nishati ya umeme ambayo ni moja ya vigezo muhimu izalishwe kwa kiasi kikubwa kufikia megawati 10,000 ili kutimiza malengo hayo.

Alisema, Wizara yake imejipanga kuhakikisha umeme wa kutosha, wa uhakika na bei nafuu unazalishwa kutoka vyanzo mbalimbali vilivyopo nchini ambavyo ni gesi asilia, maji, jotoardhi, upepo, jua, mawimbi ya bahari na makaa ya mawe.


Tangu alipoapishwa na kuanza kazi rasmi hapo Desemba 12, 2015, Waziri Muhongo amefanya ziara kadhaa kujionea na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya nishati hususan masuala ya upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu.
Post a Comment