Miaka mitano ya vuguvugu la mageuzi Misri - LEKULE

Breaking

26 Jan 2016

Miaka mitano ya vuguvugu la mageuzi Misri

Rais Abdel Fattah el-Sissi wa Misri akilihutubia taifa

Wamisri wanaadhimisha miaka mitano tangu lilipopiga wimbi la vuguvugu la maandamano ya umma lililomng'oa madarakani mtawala wa muda mrefu Hosni Mubarak.
Katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya Televisheni katika mkesha wa kuamkia maadhimisho hayo Rais wa sasa wa nchi hiyo, Abdel- Fattah el-Sissi alilipongeza vuguvugu lililouondoa utawala huo wa muda mrefu mwaka 2011 na kusema kuwa waandamanaji waliouawa wakati huo walikuwa wakipigania kurejesha misingi halali na kujenga Misri mpya.
Maadhimisho hayo yanakuja mnamo wakati ulinzi ukiwa umeimarishwa kwa kiwango cha juu katika mji mkuu wa nchi hiyo Cairo kama tahadhari ya kuzuia maandamano au mashambulizi yatakayovuruga sherehe hizo.
El-Sissi ambaye alishinda uchaguzi wa mwaka 2014 kwa kishindo alilipongeza jeshi la polisi nchini humo na kuahidi kuchukua hatua kali dhidi ya jambo llolote litakaloonekana kitisho dhidi ya utulivu wa nchi hiyo.
Jeshi la Polisi lakosolewa kwa kukiuka misingi ya haki za binaadam
Pongezi hizo kwa jeshi la polisi zinakuja huku kukiwa na malalamiko kadhaa kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo kupinga vitendo vya kikatili vinavyofanywa na jeshi hilo ikiwa ni pamoja na utesaji, kuwatia raia mbaroni pasipo sababu za msingi na kusema kuwa jeshi hilo la polisi sasa linaonekana kurejea katika enzi za utawala wa Rais Hosni Mubarak.
Ukatili wa aina hiyo wa jeshi la polisi nchini humo ndio uliosababisha malalamiko yaliyopelekea wananchi wengi wa Misri kushiriki katika vuguvugu hilo la mwaka 2011.

Rais El-Sissi alisema lengo la vuguvugu hilo la maandamano ya umma lilipoteza mwelekeo wake na kuonekana kuwa na mtizamo wa masilahi ya kibinafisi zaidi kuliko utaifa na kuonekana kuchukua mtizamo wa udugu wa kiisilamu zaidi ambalo ni kundi lililopigwa marufuku na kuchukuliwa kama kundi la kigaidi baada ya El- Sissi ambaye ni mwanajeshhi kuongoza harakati zilizouondoa madarakani utawala wa kundi hilo wa Rais Mohammed Morsi.
Alisema mapinduzi hayo yalilenga kurejesha heshima na utawala ambao wananchi wanauhitaji zaidi kwa ajili ya ustawi wa taifa hilo.
El Sissi awataka wananchi walinde Demokrasia
Aliongeza kuwa Misri ya sasa siyo ile ya jana na kuwa wanajenga taifa ambalo ni la kisasa zaidi na linalosimamia misingi ya usawa na kidemokrasia na kusisitiza kuwa demokrasia ya kweli haiji mara moja tu inakuja kwa njia ya mchakato na kutoa mwito kwa wananchi wa taifa hilo kuilinda kwa pamoja misingi ya usawa inayojengwa ili kuepuka machafuko yasiyo ya lazima katika taifa hilo.
Hata hivyo maelfu ya waungaji mkono wa kundi la udugu wa Kiislamu , pamoja na watu wengi wenye msimamo wa kati wanaharakati wanaodai demokrasi zaidi na wengine wamewekwa kizuwizini.
El Sisi amekuwa akiongoza tangu mwaka 2013 kile ambacho kundi la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linakieleza kuwa ni ukandamizaji uliopita kiasi dhidi ya wapinzani.
Chanzo:DW

No comments: