Mahakama Yamwachia Huru David Kafulila - LEKULE

Breaking

20 Jan 2016

Mahakama Yamwachia Huru David Kafulila

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemuachia huru aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kupeleka mashahidi mahakamani hapo kwa zaidi ya siku 60 kwa mujibu wa kifungo cha 25 cha kanuni ya adhabu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Slivester Kainda, katika kesi iliyokuwa ikimkabili Kafulila akidaiwa kutoa lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.

Akitoa uamuzi huo Kainda alisema: “Kesi hii ni ya muda mrefu sana na upande wa mashtaka umeshindwa kuleta mashahidi na wakati mashahidi hao wanaishi hapa Kigoma, hivyo kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuleta mashahidi ninaifuta kesi hii”.

Hakimu Kainda alifuta kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka ukioongozwa na wakili wa serikali, Shabani Masanja, kudai mahakamani hapo kuwa haukua na mashahidi na kuomba ipangwe tarehe nyingine ya kesi hiyo kutajwa.

“Mheshimiwa kwa leo (jana)hatuna mashahidi, tunaomba mahakama yako tukufu ipange tarehe nyingine ya kutajwa ili tulete mashahidi,” aliomba wakili huyo.

 Awali akisoma hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali, Shabani Masanja, alidai kuwa,  Agosti 1, mwaka 2013, majira ya jioni katika uwanja wa Rest House, kata ya Nguruka, wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma, mshtakiwa akiwa Mbunge akiwa kwenye mkutano wa hadhara alitoa lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Nyembo.

Alidai mshtakiwa huyo akiwa kwenye mkutano huo wa hadhara, alitamka kuwa “Mtu kama Hadija Nyembo unamuokota wapi na kumpa ukuu wa wilaya, unamchukua shangingi la mjini uko unasema aliwahi kuwa mkuu wa wilaya, mkuu wa wilaya akija hapa maana yake polisi wa wampigie saluti, kuna polisi wenye akili hapa kuliko huyu mkuu wa wilaya, wanampigia saluti basi tu manake hana hakili.”

Alidai lugha hiyo ilimdhalilisha mkuu huyo wa wilaya na kwamba kitendo hicho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Masanja alisema upande wa mashtaka ulipanga kupeleka mahakamani hapo mashahidi sita na kielelezo kimoja cha CD yenye maneno ya kashfa yaliyotolewa na mshtakiwa.

No comments: