Mahakama yamfutia kesi mtuhumiwa wa kupokea fedha za akaunti ya Tegeta Escrow - LEKULE

Breaking

30 Jan 2016

Mahakama yamfutia kesi mtuhumiwa wa kupokea fedha za akaunti ya Tegeta Escrow



Aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko, ameachiwa huru katika shtaka la kutuhumiwa kuwa alipokea rushwa ya Sh milioni 40.4 kutoka kwa Mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira.

Saliboko aliachiwa jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kumuona hana hatia.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, aliyesema mahakama imemuona mshtakiwa hana hatia kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha shtaka dhidi yake pasi na kuacha shaka yoyote.

“Mahakama inaona upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi bila ya shaka. Mshtakiwa (Saliboko) hana hatia, anaachiliwa huru na mna haki ya kukata rufani kwa upande ambao haujaridhika,” alisema Simba.

Alisema mshtakiwa huyo aliposomewa shtaka kwa mara ya kwanza alikana na kwamba wakati wa usikilizwaji upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Dennis Lekayo, ulileta mashahidi watatu ambao ni mpelelezi mkuu na maofisa wawili wa Benki ya Mkombozi iliyoko Ilala, Dar es Salaam.

Pia alisema mshtakiwa anatetewa na Wakili Jamhuri Johnson, alijitetea mwenyewe baada ya mahakama kumuona ana kesi ya kujibu.

Hakimu Simba alisema shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri alikuwa Mpelelezi Mkuu, Emmanuel Koroso, aliyeeleza kuwa alikabidhiwa jalada afanye upelelezi juu ya tuhuma hizo za Saliboko Oktoba 9, mwaka juzi na Mkurugenzi wa Takukuru.

Akichambua ushahidi wake, Hakimu Simba, alisema shahidi huyo alieleza alikusanya hati mbalimbali na kuhoji watu na alijitosheleza fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya Saliboko na mshtakiwa huyo hakuwa na maelezo mazuri kuonyesha namna gani alipokea fedha hizo.

Alisema mashahidi wawili kutoka Mkombozi, walithibitisha Saliboko alienda kufungua akaunti kama mteja wao na fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya mshtakiwa huyo na alizitoa mara tatu.

Kwa upande wa utetezi wa mshtakiwa Saliboko, alikubali kufungua akaunti ya Mkombozi na kuingiziwa fedha hizo na Rugemalira aliyekuwa na makubaliano naye ya kumtafutia shamba katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam ili aendeleze biashara zake.

Baada ya kuchambua ushahidi huo, Hakimu Simba alisema utaratibu wa sheria ni kwamba upande wa Jamhuri ndio wenye wajibu wa kuthibitisha mashtaka pasi kuacha shaka yoyote na sio jukumu la mshtakiwa kuthibitisha kwamba hajafanya kosa.

“Katika kesi hii, hakuna ubishi kwa upande wa Jamhuri na ule wa utetezi kwamba fedha ziliingizwa katika akaunti ya Saliboko, hivyo hakukuwa na ulazima wa kuwaleta wale mashahidi wawili kutoka Benki ya Mkombozi.

“Shahidi muhimu aliyebaki ni mpelelezi mkuu ambaye alipohojiwa na wakili wa utetezi alidai hakuna siku hata moja alienda kumuuliza Rugemalira fedha ziliingia katika akaunti ya Saliboko kwa kazi gani. 

"Kwa mujibu wa sheria za Takukuru, mtoa rushwa na mpokea rushwa wote ni wakosaji, kama kweli ilikuwa rushwa kwanini Rugemalira hakuletwa mahakamani kushtakiwa maana ni mtoaji,” alisema Hakimu Simba.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Saliboko alikuwa anadaiwa Februari 5, mwaka juzi katika Benki ya Mkombozi, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam, akiwa mkuu wa Rita alipokea Sh milioni 40.4 kupitia akaunti ya VIP Engineering ya Rugemalira ambaye alikuwa Mkurugenzi wa IPTL. 

Ilidaiwa alipokea fedha hizo kutokana na kazi yake kama bosi wa Rita wakati IPTL ilikuwa mfilisi na yeye alishughulikia hilo.

No comments: