Daraja La Kigamboni Kuanza Kutumika Machi Mosi - LEKULE

Breaking

26 Jan 2016

Daraja La Kigamboni Kuanza Kutumika Machi Mosi



Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sehemu ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga amesema daraja la Kigamboni litaanza kutumika kuanzia Machi mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kukagua hatua za ujenzi wa daraja hilo Eng. Nyamhanga amemtaka msimamizi wa ujenzi huo kuhakikisha hatua ya ujenzi iliyobaki inakamilika katikati ya mwezi februari na kuanza kazi mwanzoni mwa mwezi Machi.

“Hakikisheni Machi mosi magari yaanze kupita rasmi kwenye daraja hili na hivyo kufungua ukurasa mpya kwa wakazi wa Kigamboni ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na msongamano katika eneo la Magogoni”, amesema Eng. Nyamhanga.

Eng. Nyamhanga amesisitiza kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kuunganisha daraja la Kigamboni na barabara ya Charambe,Mlandizi hadi Chalinze ili kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji.

Amemtaka meneja wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo toka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eng. John Msemo kuhakikisha anatafuta Wakala makini atakayesimamia na kuendesha mradi huo.

Daraja la Kigamboni lenye urefu wa mita 680, unasimamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano linatarajiwa kuishi zaidi ya miaka 100 na kuwa na uwezo wa kupitisha mizigo ya tani 56 zinazokubalika katika nchi za jumuiya ya madola.

IMETOLEWA NA ;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.

No comments: