CCM Kuwashitaki Wakuu wa Shule 15 Kwa Ubadhirifu wa Fedha - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Monday, 4 January 2016

CCM Kuwashitaki Wakuu wa Shule 15 Kwa Ubadhirifu wa Fedha


JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inakusudia kuwafikisha wakuu wa shule zake 15 kwenye vyombo vya sheria kutokana na madai ya ubadhirifu wa fedha.

Akizungumza jana jijini Dar es SaIaam, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo alisema zaidi ya shule 26 walizozifanyia ukaguzi, 15 zimekutwa zikiwa na upungufu na kubwa ikiwa ni pamoja na ubadhirifu wa fedha.

“Katika ukaguzi tulioufanya, tumebaini tatizo kubwa kwenye matumizi, watu wamegeuza shule kuwa kichaka cha kutafuna fedha, sasa hawa tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria,” alisema Bulembo.

Alitoa mfano wa walimu wa shule za Tegeta, Tabata na Mwembe Tongwa ambao wameshafikishwa mahakamani kutokana na ubadhirifu. 
Aidha, Bulembo alisema taasisi yake imejizatiti katika kuhakikisha inabaki katika soko la elimu kwa kuimarisha na kutoa elimu bora katika shule wanazomiliki.

“ Kwa sasa Serikali imejipanga kuboresha shule zake, hivyo kutakuwa na ushindani wa kupata wanafunzi, ili tubakie kwenye soko ni lazima tuimarishe shule zetu,” alisema. 

Bulembo alisema pia taasisi yake imejikita katika kuanzisha vyuo mbalimbali vya elimu ya juu kwa fani mbalimbali ikiwamo kozi ya ualimu.

Akizungumzia ada elekezi, Bulembo alisema anaamini serikali itakuja na ada elekezi ambayo inaendana na wakati uliopo kwani kuendesha shule kuna gharama nyingi ambazo mzazi anachangia kupitia ada.


Serikali pamoja na kufuta ada kwa shule inazozimiliki kuanzia shule za msingi hadi kidato cha nne, inakusudia kuja na ada elekezi kwa shule binafsi lengo likiwa ni kuwapunguzia mzigo wananchi.
Post a Comment