Serikali Kuvunja Nyumba ya Waziri Mkuu wa Zamani Fredrick Sumaye. - LEKULE

Breaking

25 Dec 2015

Serikali Kuvunja Nyumba ya Waziri Mkuu wa Zamani Fredrick Sumaye.


WAZIRI Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, ameingia matatani baada ya kudaiwa kuvamia eneo la wazi na kuanza kuzungushia uzio, bila kufuata sheria na utaratibu wa ujenzi.

Eneo hilo la kiwanja namba 719/1/3 lililopo Mkiocheni, mtaa wa TPDC, lilikuwa likitumika kwa ajili ya michezo, mikutano ya kisiasa, pamoja na mikusanyiko mbalimbali ya kijamii.

Kufuatia tuhuma hizo, timu ya maofisa ardhi inachunguza uhalali wa umiliki wake, hivyo wiki ijayo majengo yaliyojengwa kwenye eneo hilo yatavunjwa, endapo itathibitika alifanya uvamizi huo.

Mbali na Sumaye, vigogo wengine wanaodaiwa kuvamia kiwanja hicho ni aliyekuwa Katibu Mkuu Mstaafu Ofisi ya Rais, Philemon Luhanjo pamoja na Mbunge wa jimbo la Rungwe, Saul Amon, ambaye ni mfanyabiashara anayemiliki maduka ya S.H. Amon.

Awali kabla ya kuvamiwa kwa eneo hilo, ilielezwa kuwa iliyokuwa kampuni ya High Precision Technology Centre (HPTCMatsutisha), ilitumika kulilinda lisivamiwe miaka ya 1970.

Hivyo mikusanyiko mbalimbali za kimichezo, pamoja na shughuli za kisiasa ilikuwa ikifanyika katika kiwanja hicho, ambako hata baada ya kampuni hiyo kufa, ililiendelea kutumika kwa shughuli za kijamii.

Taarifa zinaarifu kuwa, Sumaye anaendelea na ujenzi katika eneo hilo bila kuweka kibao chenye kuonyesha wakandarasi wanaohusika na ujenzi huo.

Lakini pia, licha ya  baadhi ya nyaraka kudai kuwa kiongozi huyo mstaafu analimiliki eneo hilo kuanzia mwaka 1998, hajawahi kulalamika kimaandishi kwenye uongozi wa mtaa kuhusu shughuli zilizokuwa zikiendelea kwenye eneo hilo.

Shughuli hizo ni pamoja na uongozi wa serikali ya mtaa kuweka kifusi, ili kusawazisha eneo hilo kuufanya uwanja utumike vizuri kwa ajili ya michezo.

Aidha wiki tatu zilizopita, Ofisa Mtendaji wa Mtaa huo Mwanaidi Omary, aliongozana na mmoja ya maofisa wa ardhi wa Manispaa ya Kinondoni hadi kwenye eneo hilo.

Ofisa huyo wa ardhi alitoa notisi ya mdomo na sio ya maandishi ya kusitishwa ujenzi huo akidai mpaka mmiliki awasilishe nyaraka serikalini.

Licha ya ujenzi huo kufanyika bila kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kutokuwepo kwa kibao kinachoonyesha mkandarasi anayehusika na ujenzi, lakini ofi sa huyo hakuchukua hatua zozote za kisheria.

Katika kutaka kujua ukweli wa mzozo huo,  barua iliyoandikwa na serikali ya mtaa kwa Halamashauri hiyo kuhoji ujenzi huo imepatikana. Barua hiyo yenye kumbukumbu namba MKT/SER/MT/ TPDC/05/2015, iliyoandikwa Desemba 11, mwaka huu na kupokelewa Desemba 14, bado haijatolewa ufafanuzi na mkurugenzi kama ilivyokuwa ikielekeza.

Kufuatia malalamiko hayo ya wananchi, Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema serikali itavunja uzio na shughuli za ujenzi zinazoendelea kwenye eneo hilo itakapobaini ukweli, ifikapo Jumatatu. 

No comments: