Serikali Kufanya Operasheni Nchi Nzima Ya Kukagua Vibali Vya Ajira Kwa Wageni - LEKULE

Breaking

29 Dec 2015

Serikali Kufanya Operasheni Nchi Nzima Ya Kukagua Vibali Vya Ajira Kwa Wageni

Serikali imeamua muda wowote kuanzia mwezi huu kuanza ukaguzi wa vibali vya Ajira za Wageni nchini, kufuatia muda wa siku 14 kuisha uliotolewa na serikali katika tangazo la utolewaji wa vibali vya kazi kwa wageni nchini lililotiwa saini Desemba 14 mwaka huu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Aiira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Jenista Mhagama (Mb), ambaye aliwataka waajiri wote nchini kwa muda wa siku hizo wawe wametekeleza matakwa ya Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya Mwaka 2015.

“Katika taarifa tuliyoitoa mwezi huu, tuliwajulisha waajiri wote wenye waajiriwa wageni ambao wana vibali vya kazi za muda (Carry on Temporary Assignment) na wale wote wasiokuwa na vibali vya ajira vilivyotolewa na kamishna wa kazi nchini kuwa wanatenda kosa. 

"Kamishna wa kazi amepewa mamlaka kutoa vibali vya ajira kwa wageni wanaotaka kufanya kazi nchini. Hivyo hakuna mamlaka nyingine yoyote inayoruhusiwa kutoa vibali vya ajira kwa wageni,” amesema Mhagama.

Amesema hayo   Tarehe 29 Desemba, 2015, Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na kikosi maalum kitakachoendesha operasheni hiyo chenye wajumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uhamiaji na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (OSHA), ikiwa lengo ni kufuatilia kama agizo lililotolewa na serikali limefuatwa na kuhakikisha taratibu zinazopaswa kufuatwa katika utoaji wa vibali vya ajira zinazingatiwa.

“Serikali ilitoa muda wa siku 14 kwa waajiri wote wawe wametekeleza matakwa ya Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.” Alisitiza Mhagama.

Mwezi Machi, mwaka huu Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya Mwaka 2015 (The Non-Citizens (Employment Regulation) Act)). 


Sheria hii imeanza kutumika rasmi tangu tarehe 15 Septemba, 2015. Sheria hiyo inaanzisha Mamlaka moja yautoaji wa vibali vya ajira kwa wageni na Mamlaka hiyo ni Kamishna wa Kazi. 


 Baadhi ya wajumbe wa kikosi maalum cha kukagua vibali vya Ajira za Wageni kutoka Idara ya Uhamiaji nchini na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (OSHA), wakifuatilia maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Bibi. Jenista Mhagama (Mb) (hayupo pichani), wakati walipokutana naye Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Desemba, 2015.

Katibu Mkuu (kazi na Ajira), Eric Shitindi akieleza jinsi operasheni ya Kukagua vibali vya Ajira za wageni kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Bibi. Jenista Mhagama (Mb) (hayupo pichani) wakati alipokutana na wajumbe wa kikosi maalum cha kukagua vibali hivyo Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Desemba, 2015.


Baadhi ya wajumbe wa kikosi maalum cha kukagua vibali vya Ajira za Wageni kutoka, Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uhamiaji nchini na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (OSHA), wakifuatilia maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Bibi. Jenista Mhagama (Mb) (hayupo pichani), wakati walipokutana naye Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Desemba, 2015.  

No comments: