Rais Magufuli Aonana Na Mjumbe Maalumu Wa Rais Paul Kagame Wa Rwanda Na Mabalozi Wa Uswisi Na Kuwait - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Thursday, 24 December 2015

Rais Magufuli Aonana Na Mjumbe Maalumu Wa Rais Paul Kagame Wa Rwanda Na Mabalozi Wa Uswisi Na Kuwait


Uswis iimeahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika Nyanja mbalimbali za maendeleo huku mkazo mkubwa ukiuelekeza katika kuendeleza elimu ya mafunzo ya ufundi stadi.

Balozi wa Uswisi hapa Nchini Mheshimiwa Florence Tinguelly Mattli, amesema hayo leo tarehe 23 Desemba, 2015 alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini  Dar es salaam.

Balozi Florence amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na kuwepo kwa miradi mingine ambayo nchi hiyo inaendelea kuitekeleza kwa kushirikiana na Tanzania, katika awamu hii Uswisi itatilia mkazo katika elimu ya ufundi stadi ilikuwawezesha vijana wanaosoma kuwa na ujuzi unaowawezesha kuzalisha bidhaa na kujipatia kipato kama ambavyo nchi ya Uswisi inafanya.

Maeneo mengine ambayo viongozi hao wamezungumzia nikuimarisha ushirikiano katika uwekezaji, ambapo Rais Magufuli amewaalika wawekezaji kutoka Uswisi kufanya biashara na Tanzania, kuimarisha huduma za bandari na pia kuongeza uwezo katika kukabilia na na vitendo vya Rushwa.

Kuhusu Sekta ya afya, Rais Magufuli ameipongeza Uswisi kwa kushirikiana na Tanzania kupitia Taasisi ya Afya Ifakara katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo kukabiliana na ugonjwa wa Malaria na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuitumia taasisi hiyo ilikusaidia juhudi za kukabiliana na magonjwa.

Wakati Huo Huo, Rais wa Jamhuri ya Muunganowa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekuta na nakufanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait hapa Nchini Mheshimiwa Jasem Al Najem Ikulu, Jijini Dar es salaam.

Katika Mazungumzo hayo, Balozi Al Najem amewasilisha salamu za mfalme  wa Kuwait Mheshimiwa Sabah Al Ahamad Al Jaber al Sabah kwa Rais Magufuli, ambaye  amempongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais waawamu ya tano na amemhakikishia kuwa Kuwait itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo ikiwemo kufadhili utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za ujenzi, Maji na Kilimo.

Miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa ujenzi C wa barabara ya Chaya – Nyahua yenye urefu wakilometa 85 kwa kiwango cha lami ambapo Tanzania imeomba ufadhili wa dola milioni 85, Mradi wa Maji wa Same - Mwanga – Korogwe ambapo Tanzania imeomba ufadhili wa dola milioni 20 na Mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Mhongo na Luhiche Mkoani Kigoma ambapo Kuwait imeonesha nia ya kuufadhili.

Aidha, Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Kuwait kwa salamu zake za pongezi na amewaalika wafanyabiashara wa Kuwait kushirikiana na Tanzania katika biashara na uwekezaji.

Katika Hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Mheshimiwa Louise Mushikiwabo aliye tumwa kuleta ujumbe maalum wa Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Katika Ujumbe huo, Mheshimiwa Kagame amemuhakikishia Rais Magufuli kuwa Rwanda itaendelea kushirikiana na Tanzania katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii hasa ikizingatiwa kuwa licha ya kuwa ni nchi jirani ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rwanda ni marafiki na ndugu wa Tanzania.

Rais Kagame pia amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi mzuri aliouonesha katika siku za mwanzo za uongozi wake wa awamu ya tano ambao amesema anauunga mkono.

Pamoja na kupokea salamu za Rais Kagame, Rais Magufuli na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda wamezungumzia mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Burundi na wote kwa pamoja wameona nimuhimu kupata suluhisho kwa njia ya mazungumzo ili wananchi waweze kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za maendeleo

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
23 Desemba, 2015

Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Al Najem Ikulu jijini Dar es salaam leo Disemba 23, 2015
Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akimsindikiza balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Al Najem baada ya kuwa na mazungumzo naye Ikulu jijini Dar es salaam leo Disemba 23, 2015.
Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akisalimiana na Mjumbe Maalum wa Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mhe. Louise Mushikwabo Ikulu jijini Dar es salaam leo Disemba 23, 2015
Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na Mjumbe Maalum wa Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mhe. Louise Mushikwabo Ikulu jijini Dar es salaam leo Disemba 23, 2015.

Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli akimsindikiza Mjumbe Maalum wa Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mhe. Louise Mushikwabo Ikulu jijini Dar es salaam leo Disemba 23, 2015. Nyuma yao ni Balozi wa Rwanda nchini.
Post a Comment